Home Uncategorized STARS NI YETU SOTE TUIPE SAPOTI, USHINDANI WA LIGI ACHA UENDELEE

STARS NI YETU SOTE TUIPE SAPOTI, USHINDANI WA LIGI ACHA UENDELEE

 


KWENYE ulimwengu wa mpira kwa sasa ni Ligi Kuu Bara pamoja na ile Ligi Daraja la Kwanza ambazo zinaendelea kuchanja mbunga kwenye viwanja tofauti.

 

Kila timu inaonyesha namna inavyosaka ushindi kwa hali na mali huku mipango ikionekana kukubali kwa timu ambazo zimejipanga.

 

 

Kwenye maisha ya mpira timu ambayo inapata ushindi ni ile ambayo itakuwa na maandalizi mazuri. Hakuna jambo jingine la kufanya wakati wa kusaka matokeo ndani ya uwanja zaidi ya maandalizi.

 

Ni ukweli ambao hauwezi kupingika kabisa ushindani wa msimu huu wa 2020/21 ni tofauti na ule uliopita wa 2019/20 kwa namna ambavyo timu zinaingia kupata matokeo ndani ya uwanja.

 

Hili linapendeza ikiwa litazidi kuendelea mpaka mwisho wa msimu kwani wengi wamekuwa wakianza na kupotea mwishoni jambo ambalo halipendezi.

 

 

 Kila timu imejipanga kwa namna yake na mwisho wa siku inapata matokeo chanya. Tunaona  namna ambavyo Azam FC imeanza tofauti kwa msimu huu.

 

Yote hayajatokea bahati mbaya bali ilikuwa ni mpangilio na hesabu katika yale ambayo wanahitaji kuyafanya. Ipo hivyo na kwa timu nyingine ambazo zinapambana nazo kupata matokeo.

 

Ligi Daraja la Kwanza nayo mambo ni yaleyale kila timu inapambana ndani ya uwanja zikisaka pointi tatu. Malengo yao ni kuona kwamba wanaweza kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao ni juhudi tu zitawapandisha.

 

 

Katika hili kila timu imekuwa ikipambana kusaka ushindi na inapata kile ambacho imekipanda. Hilo ni jambo la kwanza na jambo la pili ni kuona namna gani matokeo yanapatikana.

 

Pia  zipo timu ambazo zimekuwa na matokeo yasiyopendeza kwenye mechi zaidi ya mbili mfululizo na bado hazijashtuka kufanya maamuzi.

 

Hii ni mbaya kwa kuwa mwanzo wa ligi hesabu za wale wanaosaka ubingwa huanza kupangwa na kwa wale ambao wanajiandaa kushuka pia hesabu zao huanza kuhesabiwa.

 

Ndivyo ilivyo hata Ligi Daraja la Kwanza huku pia kila timu ina hesabu zake katika kusaka tiketi ya kupanda ligi kuu.

 

Mechi za mwanzo huwa zinakuwa hazina presha kwa kuwa kila timu inaamini kwamba ina mechi nyingi mkononi. Hili pia nalo halina maana kuliweka akilini kwa kuwa litadumu mpaka pale timu itakaposhtuka kwamba ina mechi tano mkononi.

 

 

Kasi huwa inaanza mwanzo kwa timu zote kusaka ushindi na hii itafanya iwe na mwendelezo mzuri kwa mechi zilizopo mbele.

 

 

Ni muhimu kufanya marekebisho makubwa wakati huu wa mzunguko wa kwanza ambao umekuwa na matokeo ya kushangaza ndani ya uwanja kwa timu ambazo zinacheza.

 

Wapo ambao wanapewa nafasi ya kufanya vizuri ila mwisho wa siku wanaambulia patupu na wale ambao hawapewi nafasi wanafanya maajabu ndio maisha ya mpira.

 

 Ninakumbuka msimu uliopita timu nyingi zilizinduka mzunguko wa pili wakati wakiwa na mechi chache mkononi jambo lililofanya wengi wapate matokeo ambayo hawakutarajia.

 

Makosa ambayo yamefanyika msimu uliopita ni mbaya kurudiwa tena kwani kutafanya timu zicheze kwa presha kubwa kutafuta ushindi.

 

Kwa sababu mechi za mwisho huwa na presha kubwa na kila timu inakuwa inahitaji ushindi. Inakuwa ngumu kupata ushindi kwa timu ikiwa inacheza kwa presha.

 

Ushindi hauhitaji presha bali utulivu na mbinu makini ndani ya uwanja ndizo ambazo zinabeba ushindi.

 

Tukiachana na masuala ya maandalizi ya ligi kwa mechi hizi za mzunguko wa kwanza ninapenda pia nizungumzie suala la timu yetu ya Taifa ya Tanzania pamoja na mashabiki.

 

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni yetu sote na jukumu la kila mmoja ni kuipa sapoti ili iweze kufanya vizuri iwe ni kwenye mechi ya kirafiki ama ile ya ushindani.

 

Mashabiki wamekuwa na hasira baada ya timu kupoteza mbele ya Burundi kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Mkapa.

 

Nimatokeo ambayo yanaumiza lakini hakuna tunachoweza kukibadili kwa sasa zaidi ya kufanyia kazi makosa ambayo yamepita ili kupata matokeo chanya kwenye mechi zijazo.

 

Jambo la msingi ni kwa kila shabiki kuendelea kuipa sapoti timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ili kufikia malengo ambayo yapo.

 

Zile tofauti zetu za timu kwa sasa inapofika suala la timu ya Taifa ya Tanzania ni muhimu kiziweka pembeni.

 

Kila mmoja anatambua kwamba timu pekee ambayo inasimama kwa ajili ya kuwakilisha Taifa kwenye masuala ya michezo ni Taifa Stars.

 

Rai yangu kwa mashabiki wote kwa sasa ni kuziweka kando tofauti zao na kuungana kufanya kazi moja kuipa sapoti timu ya Taifa ya Tanzania, masuala ya kuzomea na kugoma kwenda uwanjani tusiyape nafasi.

 

Mashabiki ni mchezaji wa 12 ambao wanaongeza ari ya ushindani kwa wachezaji uwepo wao ni muhimu ndani ya uwanja.

 

Imani yangu ni kwamba bado wachezaji wana ile ganzi ya kupoteza mchezo wao uliopita Uwanja wa Mkapa. Katika hili ni muhimu kutambua kwamba na mashabiki wanaumia pia.

 

Cha kufanya ni kuzidi kuongeza juhudi ndani ya uwanja. Ikifika wakati wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuitwa basi na majina yenu yawepo.

 

Isiishie kwenye kuchaguliwa wakati ule mtakapoitwa ni lazima mpambane pia kusaka ushindi mkiwa ndani ya uwanja.

 

Uzuri ni kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi na kila mmoja anaona kile ambacho kinafanyika hivyo bado nafasi ipo na imani ya mashabiki ni kubwa kwenu msiwaangushe wakati ujao.

 


SOMA NA HII  ALICHOFANYIWA MWILI JUMBA AMBAYE NI MBADALA WA MAKAMBO NDANI YA YANGA KIBOKO