Home Habari za michezo ULE MJADALA KUHUSU UWEZO WA CHICO WAIBUKA TENA….NABI AMPA MASHARTI MAGUMU YA...

ULE MJADALA KUHUSU UWEZO WA CHICO WAIBUKA TENA….NABI AMPA MASHARTI MAGUMU YA KUENDELEA KUBAKI YANGA…


Yanga inaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mechi za kumalizia msimu wa Ligi Kuu Bara pamoja na pambano lao na fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), huku kocha wao Nasreddine Nabi aliyetimkia kwao kwa mapumziko mafupi amemtumia salamu nzito mshambuliaji wake kutoka DR Congo, akimpa dili moja gumu la dakika 360.

Mshambuliaji aliyepewa masharti hayo na kutakiwa kurekebisha mambo ili mambo yamnyookee Jangwani ni Chico Ushindi, ambaye bado hajasomeka vyema kwa mashabiki tangu asajiliwe kutoka TP Mazembe kupitia dirisha dogo la usajili akipishana na Mukoko Tonombe.

Akizungumza Kocha Nabi alisema bado anaumizwa kichwa na Ushindi ambaye hajafanikiwa kuwasha moto walioutarajia wakati wanamchukua kwa mkopo kutoka Mazembe.

Nabi alisema katika kufanya maamuzi ya hatma ya mshambuliaji huyo anataka kumpa nafasi ya kutosha katika mechi tano zilizosalia kwa Yanga msimu huu, zikiwamo nne za Ligi Kuu na moja ya ASSFC ili kumsoma na kama atatoboa salama basi huenda akasalia kwa msimu ujao.

Ushindi alisajiliwa kwa mkataba wa miezi sita inayomalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akiwa hajafunga bao lolote kwenye michuano hiyo ya Ligi na ASFC, lakini kocha Nabi alisema kuna vitu ameviona kwenye miguu yake katika mechi chache alizomtumia.

“Sijaanza kumjua Ushindi hapa Yanga, namjua muda mrefu lakini kuna maisha aliyapitia Mazembe ambayo yanatupa shida kuweza kuona kile alichonacho, unapomwona mazoezini ni tofauti na kwenye mechi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Angalau mechi ya mwisho aliyocheza pale Mwanza kuna kitu kidogo alifanya, lakini kitu kibaya tunaelekea mwisho wa msimu, nafikiria kumpa hizi mechi zilizobaki kama ataweza kurudisha ubora wake.”

Nabi alisema katika mechi hizo anataka kuangalia kitu kwake kabla ya kufanya maamuzi juu ya mshambuliaji huyo kuelekea msimu ujao ambao anataka kuwa na watu wa kazi ya kweli.

Kocha huyo alisema muda mrefu amekuwa akifanya vikao vya kuwarudisha mchezoni wachezaji wake ambao wamekuwa katika hali ya kushindwa kuonyesha uwezo wao kwa kuwa bado kikosi chake kinategemea nguvu yao.

SOMA NA HII  MANCHESTER UNITED KUTUMIA MBINU HII KUINASA SAINI YA HAALAND

Ushindi katika muda ambao amekuwa Yanga amefanikiwa kutengeneza pasi moja pekee ya bao huku pia akishindwa kuonyesha uwezo mkubwa.

“Hapa Tanzania hakuna kitu ambacho kinaitwa kutoa muda, hiyo ni bahati mbaya sana kama akifanikiwa kujiuliza sasa tunaweza kuangalia kumpa muda kama ikiwa tofauti tutachukua maamuzi mengine.”