Home Habari za michezo PAMOJA NA KUVURUNDA MSIMU HUU…MASTAA WATAKOTEMWA SIMBA KUAGWA ‘KIULAYA ULAYA’…SHOW NZIMA...

PAMOJA NA KUVURUNDA MSIMU HUU…MASTAA WATAKOTEMWA SIMBA KUAGWA ‘KIULAYA ULAYA’…SHOW NZIMA ITAKUWA HIVI…


Mastaa wa Simba kwa sasa matumbo joto lipo juu kujua hatima zao msimu ujao baada ya Ligi Kuu msimu huu kubakiza mechi tano kabla ya kumalizika, lakini mabosi wao wamewatoa hofu wakiwaambia watakaotemwa watapewa mkono wa kwaheri kwa amani.

Simba imebakiza mechi tano za kufungia msimu ikiwemo kiporo na KMC, huku ikiwa nafasi ya pili katika msimamo ikikusanya pointi 51 nyuma ya Yanga yenye alama 64 baada mechi 26 ikihitaji pointi tatu katika mechi nne ili kutangaza ubingwa.

Wakati mashabiki wa Simba wakiikatia tamaa timu yao baada ya kuona msimu huu wanatoka kapa kutokana na kulitema Kombe la ASFC na ubingwa wa Ligi Kuu ukielekea Jangwani, wachezaji wa timu hiyo nao hawajajua hatima ya msimu ujao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema  kuwa kila mchezaji ambaye ataachwa atafahamishwa mapema na kuagwa kwa kupewa mkono wa kwaheri.

Try Again alisema watazungumza na kila mchezaji watakayemuacha ili wapeane mkono wa kwaheri badala ya kuwashtukiza kitu ambacho hakiwezi kuwa na afya kwa mustakabali kwa pande zote mbili.

Simba inatarajiwa kuacha wachezaji zaidi ya wanane ili kupata nafasi ya kusajili wengine kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho na Try Again alisema jana kuwa, kila mchezaji ndani ya timu hiyo anao mchango mkubwa ulioifanya timu hiyo kuwa na mafanikio makubwa ndani ya misimu minne mfululizo.

Alisema kuna ambao watawaacha kabisa ili wakajaribu maisha sehemu nyingine na wengine watawatoa kwa mkopo kwa ajili ya kulinda viwango vyao.

“Tumeteleza msimu huu ni sehemu ya matokeo ya kimpira, lakini tutarejea katika ubora wetu tuliokuwa nao siku za nyuma,” alisema Try Again.

Aliiongeza kuwa kwa sasa bado wanaelekeza nguvu kwenye mechi tano zilizosalia ili kumaliza kwa heshima kwani pointi 15 watakazopata zitawahakikishia nafasi ya pili ambayo itawahakikishia michuano ya CAF sambamba na mamilioni kutoka kwa wadhamini Azam Media.

Alisema baada ya mechi hizo ndipo watatangaza wachezaji watakaowatema au kuwatoa kwa mkopo na wale watakaosalia kikosini msimu ujao, lakini hiyo ni baada ya kuzungumza nao na kuwaaga wale watakaoachana nao au kuwatoa kwa mkopo.

SOMA NA HII  CHIKWENDE ATAJA KITAKACHOMBEBA SIMBA

Simba kwa sasa ipo chini ya kaimu kocha mkuu, Seleman Matola aliyekuwa msaidizi wa kocha mkuu aliyetimuliwa, Pablo Franco, huku mabosi wakiwa katika mchakato wa kusaka kocha mpya kwa ajili ya kuiandaa timu na mashindani ya msimu ujao.