Home Habari za michezo IMEFICHUKA….KUMBE MKATABA WA KOCHA MPYA SIMBA UNAVIPENGELE HIVI ‘KUNTU’….ALAZIMISHWA KUFANYA KAZI NA...

IMEFICHUKA….KUMBE MKATABA WA KOCHA MPYA SIMBA UNAVIPENGELE HIVI ‘KUNTU’….ALAZIMISHWA KUFANYA KAZI NA MATOLA..


IMEFAHAMIKA kuwa, Kocha Mkuu mpya wa Simba SC, Zoran Manojlović, amepewa mkataba wa mwaka mmoja wenye masharti matatu anayotakiwa kuyatimiza msimu ujao, moja ikiwemo kuipoka Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hiyo ikiwa ni saa chache tangu kocha huyo wa zamani wa Wydad Casablanca ya Morocco, Primeiro De Agosto (Angola) na Al Hilal (Sudan), atambulishwe kikosini hapo akichukua mikoba ya Mhispania, Pablo Franco.

Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, amesema kuwa, sharti la kwanza kubwa alilopewa kocha huyo ni kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya michuano ya kimataifa msimu ujao.

Aliongeza kuwa, sharti la pili ni kuhakikisha anawapoka Yanga taji la Ligi Kuu Bara na la tatu ni kulirejesha Kombe la Shirikisho la Azam Sports maarufu FA baada ya msimu huu kutolewa hatua ya nusu dhidi ya Yanga.

“Moja malengo yetu katika msimu ujao ni kuhakikisha timu inafuzu kucheza nusu fainali ya michuano ya kimataifa, hayo malengo tulimpatia na kuahidi kuifikisha huko.

“Hivyo katika masharti yetu hayo tumeyaweka kwenye mkataba wake, pia ahakikishe anarejesha makombe yote ya ndani ambayo ligi na FA.

“Kama akishindwa kufanya hayo yote, basi atakuwa amevunja mkataba wake wa mwaka mmoja wa kuendelea kuifundisha Simba, hivyo ili abaki lazima atimize masharti hayo,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Kila timu ina malengo yake, na sisi malengo yetu ni kuona tunafuzu kucheza nusu fainali katika michuano ya kimataifa.

“Hilo kocha wetu mpya analifahamu kabisa, kama robo fainali tumefika misimu miwili ya karibuni, hivyo kwa sasa tunataka kuona tunafika mbali zaidi.

“Projekti yetu ni ya muda mrefu, kama Kocha Zoran akifanya vile tunavyotaka, basi tutamuongezea mkataba.

“Kocha huyu atajiunga na timu pindi tukianza pre-season, leo (jana) tunamaliza mechi ya ligi, yeye ataendelea kusalia huko kwao akiendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na uongozi kwa njia za kisasa.

“Tukikaribia kuanza pre-season, atakabidhiwa timu akaweke mavituz yake ya Kireno na Serbia, tukirudi hapa nchini awe auwashe moto.”

SOMA NA HII  KIEMBA AFUNGUKA KILICHOWAPONZA SIMBA

HATMA YA MATOLA

Baada ya Pablo kutimuliwa, Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi, alipewa kazi ya kuwa Kaimu Kocha Mkuu, kuhusu kama ataendelea kubaki Simba, Ally amesema: “Utaratibu ambao Simba tumejiwekea ni kwamba, akija atamkuta kocha msaidizi.

“Itapendeza kocha msaidizi akiwa mzawa anayeyafahamu zaidi mazingira ya hapa nyumbani, kama tukiwa na benchi la ufundi ambalo lina kocha mkuu na msaidizi wake wote kutoka nje, watakuwa wageni na kushindwa kufanya kazi vizuri.

“Tunatarajia kwamba ataendelea kufanya kazi na kocha msaidizi mzawa, hakuna kijiji kinachokosa wazee na mzee wa Simba ni Seleman Matola.

ANAKUJA NA MAJEMBE YA MAANA

Kuhusu suala la usajili, Ally amesema: “Kocha atapendekeza baadhi ya wachezaji aliowahi kufanya nao kazi huko alipokuwa ambao anaamini akija nao Simba watamsaidia, vilevile tunashauriana naye kuhusu wale tuliokusudia kuwasajili, mwenyewe analifahamu soka la Afrika, hivyo katika hilo hakuna shida kabisa.”

MIFUMO

Kocha huyo mwenye uraia wa Serbia na Ureno, anapenda kutumia mfumo wa 4-3-3 ambao utakuwa mpya Simba. Pablo alikuwa akitumia zaidi 4-5-1.