UNAAMBIWA sasa ni wazi kuwa, usajili wa Bernard Morrison umefanya Yanga, kuingia makubaliano ya kuachana rasmi na winga wa kulia raia wa DR Congo, Jesus Moloko.
Moloko aliungana na Yanga Agosti 13, 2021, akitokea katika klabu ya As Vita ya kwao DR Congo na kusaini mkataba wa miaka miwili.
Chanzo cha uhakika kutoka Yanga kimesema kuwa, pamoja na ubora ambao umekuwa ukionyeshwa na Moloko, uongozi umelazimika kukaa naye mezani na kukubaliana kuvunja mkataba wake ili aweze kumpisha Bernard Morrison ambaye amejiunga hivi karibuni.
“Tumelazimika kufanya maamuzi magumu ya kuchana na baadhi ya nyota wetu, lengo likiwa ni kuhakikisha tunapata wachezaji watakao tusaidia zaidi kwenye michuano ijayo ya kimataifa na Ligi Kuu Bara, ambayo naamini wazi kabisa kuwa, itakuwa na upinzani mkubwa hasa baada ya kumaliza ligi bila kufungwa.
“Tayari tumeamua kuchana na Moloko, huku tukiangalia wachezaji wengine pia kama vile Makambo (Heritier) na Chiko Ushindi, ambao kwa pamoja kama tutapata mbadala wao ni lazima mmoja wao aondoke pia kwa kuwa tunahitaji nafasi zaidi,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela azungumzie ishu hiyo alisema: “Kila kitu kuhusu usajili kipo chini ya benchi la ufundi, wachezaji ambao tumekamilisha tutawatangaza hadharani na wale tutakaowaacha tutafanya hivyohivyo.