Straika wa Yanga, Fiston Mayele bado yupo mapumzikoni DR Congo, lakini ametuma salamu kwa Simba akiwaambia kwamba ameipata dawa yao na ataionyesha kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 13 kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022-2023.
Mayele aliyemaliza msimu uliopita na mabao 16, bao moja nyuma ya George Mpole wa Geita Gold, ndiye aliyefunga bao pekee lililoizamisha Simba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii ya msimu huo, lakini akashindwa kufunga katika mechi tatu zilizofuata za watani wa jadi mbili za Ligi Kuu na moja ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Akitambua kuwa msimu huu atakutana tena na Simba kwenye mechi ya Ngao, Mayele alisema katika mechi ya msimu uliopita hakupata maandalizi ya kutosha, licha ya kuwatungua, lakini safari hii anaamini atakuwa na muda mzuri wa kujifua na timu na Simba itapata tabu sana siku hiyo.
Akizungumza kutoka DR Congo, Mayele alisema; “Tunatarajia kuwa na mchezo mgumu na wa ushindani mkubwa dhidi ya Simba, ila ukweli naamini safari hii tutawashangaza zaidi.
“Timu inatakiwa kujiandaa vyema tu ili kupata kile tunachostahili. Naamini waliopo timu za taifa ndio watakuwa na ubora zaidi kutokana na kuanza mazoezi mapema tofauti na tulio majumbani,” alisema Mayele na kuongeza;
“Nakumbuka msimu ulioisha kwenye Ngao ya Jamii nilichezeshwa nikiwa sijafanya maandalizi ya kutosha kutokana na kubaki Morocco kwa janga la Uviko-19, ila namshukuru Mungu nilifunga na sasa nahitaji maandalizi zaidi ili nifanye mambo makubwa zaidi.”
Katika mchezo huo, Mayele alifunga bao dakika ya 12 na kuizamisha Simba iliyokuwa ikishikilia taji hilo kabla ya Wekundu hao pia kupoteza tena mataji ya Ligi Kuu na ASFC yaliyoenda kwa Yanga mwishoni mwa msimu.