Yanga inaendelea kujifua kambini kwa ratiba ya mazoezi ya mara mbili kwa siku lakini kocha wao Nasreddine Nabi akawaangalia mastaa wapya waliosajiliwa msimu huu kisha akasema ‘Huyu Gael Bigirimana kuja Yanga ni zaidi ya bonasi.’
Kocha Nabi alisema ameamuangalia Bigirimana kwa umakini na kutambua kwamba jamaa ni kiungo aliyekamilika anayejua kufanya kazi yake vyema eneo la kiungo.
Nabi aliongeza kwamba pasi za Mrundi huyo pamoja na akili yake ya kukaba kisasa vitaiongezea Yanga kasi kubwa eneo la kiungo msimu ujao.
“Ni mtu aliyekamilika sana, nafikiri uamuzi wake wa kuja hapa Yanga ni kama tumepata dhahabu kubwa ambayo itatupa mabadiliko makubwa katika kikosi chetu,” alisema Nabi.
“Nafikiri sio tu mashabiki wataburudika na ubora wake lakini pia hata wachezaji ambao watamuangalia kuna vitu watajifunza, anavyocheza ndivyo kiungo wa kisasa anatakiwa kucheza, ukiona jinsi anavyokaba na kupiga pasi nafsi yako inatulia.”
Aidha, Nabi amechimba mkwara mzito akisema hakuna staa mkubwa katika kikosi chake na kwamba kwasasa wanakwenda kutengeneza timu mpya.
Kocha huyo aliyechukua tuzo ya kocha bora pamoja na kuiwezesha Yanga kuchukua mataji matatu msimu uliopita, alisema kitu kikubwa kitakachompa nafasi mchezaji ni uwajibikaji wake kuanzia mazoezini na sio jina lake.
“Nafurahi kuona wachezaji wanapambana sana.”