BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imesema suala ya wachezaji wa kigeni 12 waliosajiliwa kucheza wote katika mchezo mmoja litapelekwa kwenye kamati husika na huko ndiko hatima yake itaamuliwa, imeelezwa.
Ofisa Mtendeji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo amekiri kupokea maoni mbalimbali ya wadau wa mpira wa miguu kwa ajili ya maboresho ya kanuni za Ligi Kuu msimu ujao wa 2022/2023, huku suala ya wachezaji 12 la kigeni likiwa miongoni mwa maoni hayo.
“Ni mapema sana kusema, bado tupo kwenye huo mchakato, tutapeleka kwenye vikao halali vitaamua kwa sababu hili ni jambo la kanuni siyo jambo la Bodi, wala TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), ni la wadau wenyewe, ambao ni klabu, ndiyo wataamua ni namna gani ambavyo wanataka wachezaji wa kigeni 12,” alisema Kasongo.
Mbali na hayo, ofisa huyo alisema sekretarieti ya bodi hiyo itakutana kupitia na kujidhihirisha maoni yote yaliyotumwa kama yapo sawa na kuyapekeka katika vikao husika.
“Si hilo la wachezaji wa kigeni tu, kumekuwa na maoni mengi na mitazamo tofauti kwa wadau wa soka ambayo wameyatuma kwetu, kila msimu unapoisha tunapokea maoni kwa ajili ya marekebisho,” Kasongo alisema.
Baadhi ya timu zikiwamo Simba na Yanga zimekuwa zikilalamika zinaruhusiwa kuchezesha wachezaji wageni nane kati ya 12 wanaoruhusiwa kusajiliwa, kitu ambacho kinawanyima makocha wao fursa ya kupanga vikosi kwa kuangalia uwezo wa wachezaji.