Home Habari za michezo BAADA YA KUNUSURIKA KUSHUKA DARAJA …KOCHA MTIBWA SUGAR AKATAA USAJILI WA WACHEZAJI...

BAADA YA KUNUSURIKA KUSHUKA DARAJA …KOCHA MTIBWA SUGAR AKATAA USAJILI WA WACHEZAJI VIBABU…


Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’ amesema msimu ujao wa Ligi Kuu Bara watawatumia zaidi wachezaji wao wa timu ya vijana baada ya kuona majina makubwa hayawasaidii.

Wachezaji wengi wa kikosi hicho wameondoka kikosini wengine wakitemwa ambao ni Said Ndemla na Kelvin Sabato ‘Kiduku’ waliotimkia Singida Big Stars (SBS), Salum Kihimbwa (Dodoma Jiji), Jaffar Kibaya (Ihefu), Boban Zirintusa, Shaban Kado na Baraka Majogoro huku ikidaiwa timu hiyo tayari imemsajili kipa wa zamani wa Yanga na KMC, Farouk Shikalo.

Awadhi alisema wakati mwingine ni bora kuchukua uamuzi mgumu utakaoukuumiza lakini utakaoleta matunda baadae.

“Kweli imeondoka namba kubwa ya wachezaji, kuna baadhi wameuzwa na wengine tumewaondoa na hiyo ni katika kutambua klabu ni kubwa na sio mchezaji.

“Ikumbukwe tumecheza misimu takribani miwili na wachezaji hao wote wakiwepo na hali inakuwa mbaya hivyo ukiona hupati matokeo mazuri inabidi uangalie upande mwingine,” alisema Awadh ambaye aliipa ubingwa wa michuano ya vijana timu ya vijana ya klabu hiyo hivi karibuni.

“Mwaka jana tumesajili wachezaji wengi, lakini majina yamekuwa makubwa lakini faida imekuwa ndogo katika timu, hivyo ni bora tufanye usajili wa kawaida halafu tuangalie zaidi vijana wetu.

“Sio kwamba hatutaongeza kabisa wazoefu, hapana, tunasajili wazoefu wachache lakini tunataka wachezaji wengi tupandishe kutoka timu yetu ya vijana. Bora tuanze kuhangaika na hawa vijana wadogo ambao mwisho wa siku watakwenda kutupa kitu kuliko kuangalia wachezaji wenye majina pekee.

Wakati huo huo, Awadh amemtakia kila la kheri straika wao matata, Salum Kihimbwa aliyetimkia Dodoma Jiji huku akifungua milango kwa mchezaji huyo kurejea kwa wakata miwa hao wakati wowote.

“Kihimbwa amecheza muda mrefu Mtibwa, ameitumikia vizuri klabu yetu na ameondoka kwa heshima, hajaondoka kwa ubaya.

“Anaenda Dodoma lakini najua moyo wake utabaki Mtibwa, tunamwombea afanye vizuri na sisi tukae vizuri na muda na saa yoyote tunamkaribisha kurejea nyumbani,” alisema Awadh.

SOMA NA HII  MFAUME KUUWASHA MOTO FEBRUARI, 27