Home Habari za michezo HIVI NDIVYO SIMBA ITAKAVYOVUNA MABILIONI YA CAF KUPITIA MASHINDANO MAPYA YA SUPA...

HIVI NDIVYO SIMBA ITAKAVYOVUNA MABILIONI YA CAF KUPITIA MASHINDANO MAPYA YA SUPA LIGI…


Kufanya vizuri kwa Simba kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu ya hivi karibuni kunawafanya kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuvuna mamilioni ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika michuano mipya ya Super Ligi.

Caf itafanya uzinduzi wa michuano ya Super Ligi Agosti 2023 ambayo itakuwa na zawadi ya hadi dola 100 milioni ambazo ni zaidi ya Tsh. 233 Bilioni.

Rais wa Caf, Patrice Motsepe alifichua juu ya uwepo wa michuano hiyo Jumapili kufuatia kikao cha Kamati ya Utendaji nchini Morocco ambapo masuala kadhaa yalijadiliwa, ikiwa ni pamoja na kurejea fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa mikondo miwili.

Ligi hiyo ilisisitizwa na rais wa Fifa Gianni Infantino alipotembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha miaka 80 kwa wababe wa Lubumbashi TP Mazembe mnamo Novemba 2019.

Ingawa muundo wake bado haujafichuliwa na jinsi washiriki watakavyochaguliwa, Caf ilifichua kwamba pande zinazoshiriki zitahitaji kuwa na akademi na timu ya wanawake.

Inaonekana kama ng’ombe wa pesa kwa Caf haswa kutokana na mvuto wa klabu kubwa kama vile miamba ya Misri Al Ahly na Zamalek, Wydad ya Morocco na Raja Casablanca, Esperance ya Tunisia, TP Mazembe na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.

Simba inaweza kuwa kwenye kundi hilo kutokana na kutinga kwao mara tatu katika hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa, Shirikisho na Ligi ya Mabingwa ndani ya misimu ya hivi karibuni.

Japo wapo ambao wanaipa hata Yanga nafasi kutokana na sababu za kibiashara.

Caf inahisi inaweza kuzalisha zaidi ya dola milioni 200 kwa udhamini huku nusu ya fedha hizo zikielekezwa kwenye michuano hiyo huku zingine zikielekea katika maendeleo ya miundombinu na kukuza soka la Afrika.

Wakati huo huo, Motsepe alijiondolea lawama kufuatia mzozo uliotokana na Morocco kuandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka huu ambapo timu ya nyumbani Wydad iliifunga Al Ahly 2-0 katika mchezo ambao miamba hiyo ya Misri ilitishia kususia kutokana na uchaguzi wa uwanja.

SOMA NA HII  SIMBA WATUA KIBABE BENINI...WAANZA KWA TAMBO NA MIKWARA..AHMED ALLY AUNGURUMA...

“Hili halitatokea tena. Ni kitu ambacho nilirithi, ni kitu ambacho sikuweza kubadilisha, uamuzi ulichukuliwa mbele yangu. Tutakuwa na fainali ya mikondo miwili tena,” alisema Motsepe, huku akithibitisha kurejea katika mfumo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa mikondo miwili. Nini maoni yako kuhusiana na mashindano haya unadhani yatainua soka la Afrika haswa kwa wakati huo ambao ligi nyingi zinaanza? Tutumie kwenye namba yetu.