Home Habari za michezo KISA TUZO YA SAKHO….MABOSI SIMBA ‘WAVIMBA MASHAVU’…WATUMA UJUMBE KWA YANGA…

KISA TUZO YA SAKHO….MABOSI SIMBA ‘WAVIMBA MASHAVU’…WATUMA UJUMBE KWA YANGA…


Kitendo cha mastaa wakubwa wa Afrika na Dunia akiwemo Jay Jay Okocha wa Nigeria na Sadio Mane wa Senegal kumsifu staa wa Simba, Pape Osmane Sakho kimewapa kiburi viongozi wa Wekundu hao ambao wametambia Yanga kwamba: “Sisi siyo saizi yenu.”

Hali hiyo imehamia mpaka kwa wanachama ambapo juzi kwenye makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi gumzo kuanzia majira ya saa 4 asubuhi mpaka jioni ilikuwa ni tuzo ya goli bora Afrika 2022 aliyopata staa wao.

Sakho alishinda tuzo hiyo baada ya kuibuka kinara dhidi ya Gabadinho Mhango wa Malawi na klabu ya Orlando Pirates na nyota wa Wydad Casablanca na Morocco, Zouhair El Moutaraji.

Bao hilo la Sakho ambalo limeshinda tuzo ya goli bora la mwaka alifunga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Asec Mimosas kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 13.

Sakho alifunga bao hilo kwa staili ya tiktak akiunganisha kwa mguu wa kulia krosi iliyopigwa na beki wa Simba, Shomari Kapombe aliyepokea mpira uliotokana na kona fupi iliyochongwa na Rally Bwalya. Licha ya CAF kufanya siri fedha za tuzo hiyo wakimalizana na mhusika juu kwa juu lakini imedokezwa kwamba ni Sh20milioni taslimu.

Tuzo hiyo iliyoipa Simba na Tanzania sifa kubwa duniani, alikabidhiwa na nyota wa zamani wa Nigeria na PSG, Jay Jay Okocha lakini ilimpa fursa ya kukutana na kupiga picha ya pamoja na mshindi wa tuzo ya mchezaji bora Afrika na nyota wa Senegal na Bayern, Sadio Mane.

Kana kwamba haitoshi, tuzo hiyo ilikuwa ni fursa ya kumkutanisha na kocha wa Senegal, Aliou Cisse ambaye alikuwa mshindi wa tuzo ya kocha Bora Afrika upande wa wanaume.

Ushindi wa Sakho, umemuibua Rais wa Senegal, Macky Sall ambaye amempongeza nyota huyo wa Simba na washindi wengine wa tuzo kutoka katika taifa lake.

“Mavuno ya aina yake kwa Senegal katika tuzo za Caf 2022. Kupitia ushujaa na tuzo zenu kocha Aliou (Cisse), Sadio Mane, Pape Matar Sarr, Pape Sakho na wengine waliochaguliwa, mmeifanya Senegal hii kuwa taifa la kuvutia na kuheshimika kimpira. Hongereni.”

SOMA NA HII  TWAHA KIDUKU: NGUMI ZANGU ZINAUMA

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, kocha wa Senegal, Aliou Cisse ameahidi kumuita kikosini nyota huyo wa Simba kama ilivyothibitishwa na mtandao wa www.senenews.com.

“Goli la aina yake ambalo limemfanya Alhamisi hii ashinde tuzo ya goli bora katika tuzo za Caf. Fursa ambayo imemfanya kocha Aliou Cisse kumwambia kwamba muda mfupi ujao atamualika katika timu ya taifa,” umeripoti mtandao huo. Ingawa wachambuzi wanasema kuna changamoto kubwa ya mchezaji huyo kupata namba kutokana na utitiri wa mastaa wa Senegal Ulaya.

Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji, amempongeza Sakho akisema kupitia akaunti yake rasmi ya Instagram: “Asante kwa kuleta heshima ya kipekee kwa Simba na Tanzania. Tuzo hii imezidi kuonyesha namna gani Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wenye viwango vikubwa.”

OFA ZAMIMINIKA

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, muda mfupi baada ya nyota huyo kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya goli bora, wamekuwa wakipokea ofa nyingi kutoka ndani na nje ya Afrika zikimhitaji Sakho.

“Ukweli ni kwamba Simba tumepokea simu nyingi sana, klabu wamekuwa wakihitaji tumalize biashara. Wengine wanamfuata mchezaji wakitaka tumalizane. Presha ni kubwa sana kiukweli ila mwisho wa siku tutazipima.‚

“Utamaduni wetu kama Simba ni kuwapa fursa wachezaji wetu, ikitokea wamepata ofa nzuri hakuna shida. Nikikwambia nina ofa zaidi ya mbili kwa ajili ya Kanoute utakubali? Wachezaji wengi wana ofa kutoka nje, ila lazima tutakaa chini kutafakari,” alisema Barbara.

Kabla ya Sakho kushinda tuzo hiyo, Al Hilal ya Sudan inaripotiwa ilitenga kiasi cha Dola 400,000 (Sh 932 milioni) kwa ajili ya kumsajili Sakho ofa ambayo Simba waliikataa lakini baada ya jana mfano wa timu nyingine zilizoonyesha nia ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji ni Wydad Casablanca na Raja Casablanca. Sakho alitoa shukrani; “Asanteni Watanzania, asanteni mashabiki wa Simba, asanteni wachezaji wote, nimefurahi sana.”