Home Habari za michezo KWA YANGA HII MPYA WASHINDWE WENYEWE TU KUTOBOA CAF…HAYA HAPA MAMBO 5...

KWA YANGA HII MPYA WASHINDWE WENYEWE TU KUTOBOA CAF…HAYA HAPA MAMBO 5 MAKUBWA YATAKAYOWABEBA…


Kocha wa Yanga, Nasredinne Nabi amekaririwa akisema kwamba msimu huu wamedhamiria kufanya vizuri katika michuano ya CAF tofauti na msimu uliopita ambao walitolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu ulioisha Yanga ilitolewa mapema baada ya kuchapwa nyumbani bao 1-0 na kupata matokeo kama hayo ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria, jambo ambalo halikuakisi mafanikio ya kitaifa ambayo walikuja kuyapata mwisho wa msimu wakitwaa mataji yote matatu Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Kwa msingi wa kauli ya Nabi, haya hapa mambo matano yanayoweza kuibeba Yanga kwenye michuano ya CAF, msimu huu.

AINA YA USAJILI

Yanga haijabomoa sana kikosi, imewapunguza baadhi kama Yassin Mustapha aliyetimkia Singida Big Stars (SBS), Paul Godfrey (SBS), Said Ntibazonkiza ‘Saido’, Yacouba Sogne (Geita Gold), Balama Mapinduzi na pia inasemekana wanaweza ikaachana na Deus Kaseke, Chico Ushindi, Heritier Makambo na Erick Johora.

Walioingia ni kiungo wa ushambuliaji Aziz Ki kutoka Asec Misosas, winga Benard Morrison kutoka (Simba), beki wa timu ya taifa ya DR Congo, Joyce Lomalisa, kiungo kutoka Burundi, Gael Bigirimana na mshambuliaji Lazarous Kambole (Kaizer Chief ya Afrika Kusini).

Mastaa waliowasajili ni wazoefu wa michuano ya CAF, huduma yao inategemewa kuibeba Yanga kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajia kuanza Septemba.

UONGOZI MPYA

Viongozi wapya wa Yanga walisimikwa madarakani Julai 9, Rais ni Mhandisi Hersi Said na makamu wake ni Arafat Haji ambao kwenye kampeni zao waliahidi kuhakikisha timu inafanya vyema CAF.

Ni wakati mwafaka wa kuzifanya ahadi zao kwa vitendo hasa kipengele cha Yanga iwe klabu ya kwanza kunyakua taji la Afrika.

“Tunataka Yanga iwe klabu ya kwanza kunyakua ubingwa wa Afrika, tutasajili wachezaji wenye viwango vikubwa, vitakavyoendana na uhalisia wa mashindano hayo,” nukuu ya Arafat.

MORALI YA UBINGWA

Yanga imetoka kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ulioisha na kufikisha taji la 28, hilo linatawapa morali wachezaji kuhitaji rekodi anga za kimataifa kama walizoweka watani wao Simba ambao walifika hatua ya robo fainali msimu ulioisha.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA SC KINACHOANZA DHIDI YA ASEC MIMOSA

KOCHA YULEYULE

Nabi hajasaini mkataba mpya na kuna maswali kuhusu ukimya wake na benchi zima la ufundi kama litaendelea kuwepo msimu ujao. Lakini kwa kuwa uongozi haujatoa tamko tofauti, matarajio ni kwamba Yanga itaendelea na Nabi, msaidizi wake Cedric Kaze na benchi zima la ufundi lililoiongoza timu hiyo ya Jangwani kutwaa ubingwa kwa kucheza mechi 30 bila ya kupoteza na kuweka rekodi binafsi ya mechi 37 mfululizo hadi sasa bila ya kupoteza (kuanzia msimu wa 2020-21) katika ligi. Wamebakiza mechi moja kuifikia rekodi ya muda wote (mechi 38) inayoshikiliwa na Azam FC.

MZUKA MASHABIKI

Mashabiki ni mchezaji wa 12, kitendo cha Yanga kunyakua taji la Ligi Kuu na ASFC msimu ulioisha kinawafanya wawe na morali ya kuisapoti timu yao, kuhakikisha wanawapa moyo mastaa wao.

Kutokana na namna Yanga inavyosajili, staa wa zamani wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anatarajia kuwaona wachezaji wakifanya makubwa CAF.

“Kitu kizuri nilichofurahia kikosi hakijapanguliwa sana, wachezaji wamezoeana na wameongezwa wazoefu wa michuano ya CAF, binafsi natarajia kuona timu yangu ikifanya makubwa msimu huu,” anasema.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ anasema anatarajia kuona wachezaji wakiandika rekodi CAF.

“Wamekaa pamoja, itawabeba sana,” anasema.