Home Habar za Usajili Simba WAKATI OKWA AKITUA NA MZUKA WA KINIGERIA SIMBA…MANZOKI AIBUKA NA KUKOLEZA UKAKASI...

WAKATI OKWA AKITUA NA MZUKA WA KINIGERIA SIMBA…MANZOKI AIBUKA NA KUKOLEZA UKAKASI WA DILI LAKE…


Kiungo mpya wa Simba, Mnigeria Nelson Okwa wikiendi iliyopita aliiaga timu aliyokuwa akiichezea ya Rivers United kibabe kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kisha mapema anaanza mchakato wa safari ya kwenda kuanza maisha mapya ndani ya kambi ya Simba iliyopo Ismailia, Misri.

Okwa ni mmoja ya nyota wapya waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha hili la usajili litakalofungwa Agosti 31 na mara baada ya mechi ya mwisho na Rivers iliyoitoa Yanga kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, aliwaaga wenzake na benchi la ufundi na fasta jana alichukua usafiri wa ndege kutoka Mji wa Port Harcourt alipokuwa na timu yake ya Rivers kisha akatua Abuja kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusafiri kwenda kambi ya Misri.

Taarifa kutoka Nigeria, zinasema Okwa alibidi afike kwanza Abuja kutokana na kuhakikisha anapata visa ya kuingia Misri ilipo kambi ya timu yake mpya ya Simba ambayo kwa mujibu wa Kocha Zoran Maki itakuwa ya wiki tatu na itacheza mechi zisizopungua tano kabla ya kurejea nchini Agosti 5.

Inaelezwa muda wowote kuanzia sasa kama Okwa atapata visa atatumiwa tiketi ya ndege na mabosi wake wapya wa Simba kisha atatua Misri kwa ajili ya kutambulishwa kama mchezaji mpya wa timu hiyo.

Baada ya zoezi hilo la kutambulishwa kukamilika atajiunga moja kwa moja kwenye mazoezi na wachezaji wenzake .

Okwa  alikiri yupo Nigeria kwa ajili ya mambo yake mengine na kama atakuwa mchezaji mpya wa Simba msimu ujao basi hilo si jukumu lake kuweka wazi.

“Ishu ya kuwa mchezaji mpya wa Simba basi viongozi wangu ndio wana haki ya kuliweka hilo wazi lakini kwa sasa nipo kukamilisha mambo yangu binafsi hapa Abuja, hayo mengine tuyaache kwanza,” alisema Okwa anayefahamika nchini kutokana na kiwango bora alichoonyesha wakati alipocheza mechi mbili dhidi ya Yanga.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kikosi chao bado hakijamaliza zoezi la usajili kwani kuna wachezaji wengine wapya kama si wawili basi watatu watawatangaza baada ya kukamilisha taratibu zao.

SOMA NA HII  PHIRI AJIKUTA NJE YA LIST.... ISHU NZIMA IKO HIVI

“Viongozi wanaendelea na zoezi la usajili, kama likikamilika ndani ya muda mfupi tutawatangaza wachezaji hao wawili au watatu wapya ambao watajiunga nasi huku Misri. Mashabiki waendelee kutuombea dua ili tufanye vizuri msimu ujao katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa,” alisema.

ISHU YA MANZOKI

Juzi Ijumaa, Simba ilipata ugeni baada ya mshambuliaji kutoka Vipers ya Uganda, Cesar Lobi Manzoki kutua Dar es Salaam akitokea mapumzikoni kwao DR Congo baada ya kumaliza msimu akiwa kwenye mafanikio makubwa binafsi na timu kiujumla, huku kubwa ikiwa ni kushughulikia dili lake la kutua Msimbazi.

Hii ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo kutua nchini kimya kimya, kwani awali alitua na kusainishwa mkataba wa miaka miwili na Simba na safari hii amekuja ili kupigwa tafu juu ya kupata barua ya kuruhusiwa kuondoka kutoka Vipers ambao wameamua kuweka ngumu kwa madai bado wana mkataba naye, japo mwenyewe anasisitiza umeisha mwisho wa msimu huu.

Chanzo chetu makini kutoka Uganda kilieleza Manzoki alisaini mkataba wa miaka miwili uliomalizika mwisho wa msimu huu, japo mabosi wa Vipers wameamua kukomaa naye na kumfanya ashindwe kuungana na wenzake Misri, licha ya jina lake kuwepo katika orodha ya watu 48.

“Manzoki ni mchezaji huru kwani mkataba wake wa miaka miwili amemaliza ila bahati mbaya nakala ya mkataba wake aliiweka kwenye simu ambayo ilipotea, hivyo hana ushahidi na hapo Vipers wamemchomekea mwingine wa miaka miwili,” kilisema chanzo makini kutoka Uganda.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya Simba zinasema baada ya klabu kupambana kwa siku tatu ili kupata kibali cha kuruhusiwa kumtumia Manzoki, iliamua kumleta nchini ili washughulikie kwa kupitia wanasheria ili kupata kibali kutoka FUFA (shirikisho la soka la Uganda) na Vipers.

Manzoki, alipotafutwa alisema kwa kifupi; “Tusubiri kuna mambo ya kimsingi yanawekwa sawa, yakimalizika hayo itafahamika timu nitakayoitumikia msimu ujao, kwa sasa niache tu kwanza.”