Home Habari za michezo KWA YANGA HII YA MAYELE, AZIZI KI NA MORRISON …YALE MABAO YA...

KWA YANGA HII YA MAYELE, AZIZI KI NA MORRISON …YALE MABAO YA SIMBA MISIMU ILIYOPITA KUHAMIA JANGWANI…


Mastaa wa Yanga, Fiston Mayele na Aziz Ki kama watacheza kitimu msimu ujao (2022/23), safu yao itatengeneza idadi kubwa ya mabao, kitu ambacho kimewahi kufanywa na wachezaji wa Simba, Luis Miquissone na Clatous Chama (2020/21).

Msimu wa 2020/21 Luis na Chama walichangia mabao 42 kati ya 78 ya timu nzima, ingawa kinara wa mabao 16 alikuwa ni nahodha wao John Bocco.

Chama alimaliza na mabao nane na asisti 15, wakati Luis alimaliza na mabao tisa na asisti 10, wawili hao walikuwa mwiba dhidi ya wapinzani wao na timu ilikuwa na uhakika wa kupata matokeo ya ushindi kupitia wao.

Kuondoka kwa Luis aliyeuzwa Al Ahly ya Misri na Chama kujiunga na Berkane ya Morocco kabla ya kurejea tena ndani ya kikosi hicho, kuliacha pengo kubwa katika nafasi zao.

Msimu uliyoisha Yanga ilinyakua taji la Ligi Kuu Bara, huku Mayele akiwa kinara wa mabao 16 ndani ya kikosi hicho, hivyo kuongezwa kwa Aziz Ki anaweza kucheza winga ya kushoto, kulia, namba tisa na 10 ni faida kwa klabu hiyo kuwa na watatengeneza mabao wengi.

Yanga ilimsajili Aziz Ki kwa mkataba wa miaka miwili, kutoka  ASEC Mimosas ambako alifanya vizuri, hiyo ndiyo sababu ya mashabiki wa Wanajangwani kuusubiri utambulisho wake hadi saa 9:00 usiku. Ujio wa Aziz Ki na uwepo wa Mayele, ulimuibua mcheka na nyavu wa zamani Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyesema endapo mastaa hao wakiamua kucheza kitimu anaona watakuwa na kombinesheni hatari msimu ujao.

“CV za Aziz Ki zinaonyesha ni mchezaji mzuri, Mayele tayari ameonyesha umahili wake wa kufunga, hivyo naiona Yanga yenye washambuliaji hatari zaidi kwa Ligi Kuu ijayo,” alisema.

Hoja yake iliungwa mkono na straika wa zamani wa timu hiyo, Malimi Busungu aliyesema anaiona timu hiyo inazidi kuimalisha safu yake ya mbele, hivyo anatarajia kuiona inazalisha mabao mengi zaidi.

“Kuhusu Aziz Ki nasubiri aonyeshe uwanjani ila kwa CV yake anaonekana ni mchezaji mzuri na alichokifanya Mayele kipo wazi, wakielewana katika uchezaji kama ilivyokuwa kwa Luis na Chama walivyofanya vizuri msimu wa 2020/21 basi watafanya vizuri zaidi,” alisema.

SOMA NA HII  SIMBA YATUMA MAJINA 31 CAF..CHIKWENDE ATEMWA..WAONGEZA VIFAA VIPYA VIWILI KIMYAKIMYA...