Home Habari za michezo TANZANIA YAOMBA KUANDAA AFCON 2027…SERIKALI YABARIKI…VIWANJA VYA SIMBA NA YANGA KUTUMIKA…

TANZANIA YAOMBA KUANDAA AFCON 2027…SERIKALI YABARIKI…VIWANJA VYA SIMBA NA YANGA KUTUMIKA…


Tanzania inatarajia kutumia fursa ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika utakaofanyika jijini Arusha mwezi Agosti, kuthibitisha ipo tayari kuwasilisha ombi la kuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ 2027.

Tanzania haijawahi kuwa mwenyeji wa Fainali hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 1957, licha ya kuwahi kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa Fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019 zilizofanyika jijini Dar es salaam.

Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mohamed Mchengerwa ameweka wazi dhamira ya Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kuwathibitisha utayari wa kuwa mwenyeji kwa mwaka 2027.

Waziri Mchengerwa aliyasema hayo juzi Alhamis (Julai 07), alipokua akihutubia kwenye hafla ya Utoaji Tuzo kwa Timu, Wachezaji, Makocha na Waamuzi waliofanya vizuri msimu wa 2021/22 uliofikia tamati mwezi Juni.

“Mpango wa Serikali ni kuandaa mashindano ya AFCON 2027 hapa hapa Tanzania na inawezekana. Sera ya michezo inavitaka vilabu kujenga viwanja vyao vyenyewe.”

“Viwanja vinavyofanyiwa ukarabati na Serikali ni mkakati kwa ajili ya mashindano makubwa. Naomba vilabu viwekeze kwenye kujenga vilabu vyao vyenyewe. Kuna vilabu vipo tangu kabla ya Uhuru, vinashindwaje kujenga viwanja vyao vyenyewe.” Alisema Mchengerwa

Viongozi wa vilabu wawe wabunifu, kama wanachama wapo tayari kuchanga changisheni.

Naiagiza BMT na TFF waniandalie kikao wiki ijayo na Watendaji wakuu wa vilabu ili tuzungumze kwa nini vilabu vinashindwa kuwa na viwanja vyao vyenyewe.

Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ umepangwa kufanyika Agosti 10 jijini Arusha, na tayari Rais wa Shirikisho hilo Patrice Motsepe ameshathibitisha hilo alipozungumza na Waandishi wa Habari mjini Casablanca-Morocco Jumapili (Julai 03).

Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ 2023 zitafanyika nchini Ivory Coast na zile za mwaka 2025 zimepangwa kuunguruma nchini Guinea.

SOMA NA HII  SIMBA YANGA VICHEKO TU