Home Habari za michezo USAJILI WA AZIZ KI YANGA WAMUIBUA YACOUBA SOGNE…ABUKA NA HOJA HIZI JIPYA...

USAJILI WA AZIZ KI YANGA WAMUIBUA YACOUBA SOGNE…ABUKA NA HOJA HIZI JIPYA KUHUSU UWEZO WAKE NA SOKA LA TZ…


Achana na utambulisho wa Stephane Aziz KI uliofanywa usiku mnene wa kuamkia jana baada ya juzi  kushuhudia ujio wake ulivyojaa umafia, rekodi za staa huyo zimekoleza mzuka Jangwani.

Kwa mujibu wa takwimu za klabu aliyotoka ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, msimu uliomalizika hivi karibuni, Aziz KI ameichezea timu hiyo mechi 29 kati ya 38 zilizoipa taji lao la 28 la Ligi Kuu ya kwao.

Katika mechi hizo amefunga mabao 10 na kuasisti sita, akiwa ametumia jumla ya dakika ya 2234 akipiga pasi 1074, huku akikokota mpira mara 87, kitu kilichomfanya rafiki na raia mwenzake anayepishana naye Yanga, Yacouba Sogne kushindwa kujizuia na kumsifia vilivyo.

Rekodi zinaonyesha pia kwenye mechi za kimataifa anatisha kwani katika mechi 10 za Kombe la Shirikisho Afrika jamaa alitupia nyavuni mara nne.

Aziz KI ametambulishwa juzi kwa mkataba wa miaka miwili anaungana na Bernard Morrison, Lazarous Kambole, Gael Bigirimana na Joyce Lomalisa ambao wote kwa pamoja wamesajiliwa katika dirisha hili la uhamisho.

Sogne aliyeshindwa kufanya vizuri ndani ya timu hiyo msimu uliopita kwa kuwa majeruhi na anayepelekwa kwa mkopo, Geita Gold, alisema staa huyo mpya amekoleza mzuka Jangwani, lakini ana kazi kubwa ya kufanya ili kujitengenezea ufalme ndani ya timu hiyo.

“Ni mchezaji mzuri ameonyesha uwezo kwenye mashindano ya ndani na kimataifa kila mmoja ameshuhudia, nimemsimulia soka la Tanzania na mashabiki namna wanavyotaka matokeo ya haraka ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anakuwa bora kama matarajio ya watu yalivyo,” alisema Sogne ambaye ni raia wa Burkina Faso kama alivyo Aziz KI na kuongeza;

“Aziz KI ni mchezaji mkubwa na bora kwenye kikosi cha Yanga kwasasa pia kwenye nafasi anayocheza ni yeye pekee anayetumia mguu wa kushoto na ni mzoefu, sina shaka naye pia amekuwa muumini wa kuuliza mara kwa mara maisha ya Tanzania kabla ya kutua, naamini atafanya vizuri na kuendana na kile kinachotarajiwa.”

Yacouba alisema usajili walioufanya Yanga katika dirisha hili la usajili linaloendelea ni mzuri na anatarajia kuiona Yanga ikiwa bora ndani na nje kutokana na timu kujaza wachezaji wenye uwezo tofauti zaidi ya mmoja kila eneo.

SOMA NA HII  KISA USHIRIKI WA SIMBA KIMATAIFA...KLABU LIGI KUU ZAJIKUTA NA MSALA WA KUFA MTU...ISHU IKO HIVI...

Akizungumzia mkataba wake na Yanga, Yacouba alisema bado ni mchezaji wa timu hiyo lakini jukumu la yeye kuondoka au kubaki anauachia uongozi ambao ndio utakaotoa taarifa na sio yeye.

“Nimesikia mambo mengi kunihusu, ninachoweza kukwambia sasa ni kwamba mimi ni mchezaji wa Yanga hadi hapo uongozi utakapotoa taarifa rasmi za kuniacha au kunitoa kwa mkopo kama wengi wanavyoripoti,” alisema mchezaji huyo mwenye uzoefu mkubwa.