Home Habari za michezo YANGA YACHELEWA..COASTAL UNION WAFUKIA KITU UWANJANI….

YANGA YACHELEWA..COASTAL UNION WAFUKIA KITU UWANJANI….


KLABU za Yanga na Coastal Union zimepewa onyo kali na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu kutokana na kukiuka kanuni mbalimbali zinazoendesha mpira wa miguu, moja ikionywa kwa uchelewaji na nyingine kuchimba na kufukia kitu kisichojulikana uwanjani.

Yanga imepewa onyo kwa uchelewaji kwani ilishindwa kufika kwa wakati husika kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, huku Coastal  nao wakipewa pia onyo kwa kufukia kuchimba na kufikia kitu kisichojulikana uwanjani, kuashiria mambo ya kishirikina kwenye mechi ya dhidi ya Namungo FC.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi imesema, katika kikao chake cha Julai 6 mwaka huu, ilipitia mwenendo wa matukio mbalimbali ya Ligi Kuu na kufanya maamuzi hayo.

“Mechi namba 214, Yanga ilicheza dhidi ya Coastal na kushinda mabao 3-0. Kwenye mechi hiyo Yanga imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani. Ilifika saa 1:12 usiku badala ya saa 1:00 usiku kuelekea mchezo tajwa uliochezwa Mei 15, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa kanuni 17: (15 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.” Ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imesema kwenye mechi namba 217, ambayo Coastal Union ilishinda bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa Ilulu, mchezaji Bigirimana Blaise wa Namungo FC, amepewa onyo kali kwa kuonekana akitupa vipande vya ndimu kwenye upande ilipokaa timu ya Coastal, huku mchezaji mwenzake Hamisi Mgunya naye akipewa onyo kwa kosa la kwenda kwenye goli la Coastal Union na kumwaga kimiminika kutoka kwenye chupa kuelekea mchezo huo uliochezwa Juni 20, 2022.

“Pia klabu ya Coastal Union imepewa onyo kali kwa kosa la wachezaji wake kuzingira eneo la katikati ya uwanja na kuchimba shimo dogo, kisha kufukia kitu kisichojulikana.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa kanuni ya 47 (1) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.” Ilimaliza taarifa hiyo ya Bodi ya Ligi.

SOMA NA HII  MCHONGO NI KUCHEZA KASINO| EXPANSE INALIPA ZAIDI....