ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amezichambua timu kongwe zinazovaana leo kwa kusema Simba ipo vizuri kwa upande wa beki na washambuliaji, huku Yanga ikiwa haijakaa sawa upande wa beki.
Simba na Yanga zinashuka dimbani leo uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ngao ya Jamii ukiwa ni ufunguzi wa ligi kuu msimu wa 2022/23.
Rage amesema kuwa, kwa jinsi alivyoviona vikosi vyote viwili licha ya kufanya usajili mzuri amebaini beki ya Yanga kutokuwa vizuri zaidi ya Simba licha ya kuwa na kikosi kizuri.
“Mechi ya leo itakuwa ngumu kutokana na usajili wa timu zote mbili ulivyofanywa, mara nyingi huwa ni nyepesi kutabiri mshindi, lakini mechi ya kesho ‘ leo’ ni ngumu kutabiri kwa sababu mbili.
“Moja timu zote mbili zimesajili vizuri, pili wanao wachezaji wazuri lakini niseme wazi si kwa ushabiki naweza kutoa ‘advantage’ kwa Simba ambao wamesajili washambuliaji wazuri na beki ipo vizuri pia kwa jinsi nilivyoiona ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya St. George.
“Yanga yenyewe ina kikosi kizuri sana kwa upande wa washambuliaji, lakini beki haipo sawa kutokana na mechi walizocheza ukiangalia ile ya mwisho dhidi ya Coastal Union na hii dhidi ya Vipers ya Uganda ambayo walifungwa 2-0.
“Mara nyingi mechi za Simba na Yanga huwezi kuzitabiri nani anaweza kushinda lakini natoa nafasi kubwa kwa Simba,” alisema Rage.