Home Azam FC AZAM FC WANOGEWA NA KAMBI YA MISRI…WAHAMIA CAIRO KUSAKA MISULI ZAIDI YA...

AZAM FC WANOGEWA NA KAMBI YA MISRI…WAHAMIA CAIRO KUSAKA MISULI ZAIDI YA KUKIWASHA LIGI KUU…


KIKOSI cha Azam FC kimeondoka katika  mji wa El Gouna kuelekea Cairo ili kusaka mechi nyingine za kirafiki na timu kubwa kwa ajili ya kumpa nafasi kocha kufanya tathmini ya kikosi baada ya mazoezi ya wiki mbili yanayoendelea huko nchini Misri.

Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zacharia ‘Zaka’, alisema Kocha wao, Abdihamid Moallin amefanya kazi kubwa kuitengeneza timu hiyo na sasa anataka aangalie matokeo yake kwa kuhitaji mechi dhidi ya klabu kongwe tofauti na zile walizocheza awali.

“Wiki ya kwanza (kocha) alikuwa na kazi ya kuitengeneza safu ya ulinzi, iliyofuata akaanza kusuka mastraika na sasa anataka angalau mechi mbili kubwa na siyo zile ambazo tumecheza. Mfano tuliyocheza nayo Grand FC tukashinda bao 1-0 ni ya Daraja la Pili, kwa hiyo tunatoka El Gouna na kwenda Cairo kusaka mechi angalau mbili kabla ya kurejea nyumbani,” alisema Zaka.

Ofisa huyo alisema endapo itashindakana kupata mechi hata moja, tayari wamefanya mipango ya kucheza mchezo na timu kutoka Kuwait na baada ya hapo kocha atajua kikosi chake kilipofikia.

Azam imeweka kambi yake Misri kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali, ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho Afrika.

Mpaka sasa kikosi hicho kimecheza mechi mbili tangu ambapo ya kwanza ilikuwa ni dhidi ya Wadi Degla ya huko na kuchapwa bao 1-0 huku mchezo wake wa pili ikishinda goli 1-0 dhidi ya Grand FC, mfungaji akiwa ni Mzimbabwe Prince Dube.

Azam FC itafungua pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara Agosti 17, mwaka huu kwa kuwakaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU