Home Habari za michezo BALAA LA KAMBOLE MAZOEZINI LAMFANYA NABI KUCHUKUA MAAMUZI MAGUMU YANGA….ATENGENEZA KOMBINESHI MATATA…

BALAA LA KAMBOLE MAZOEZINI LAMFANYA NABI KUCHUKUA MAAMUZI MAGUMU YANGA….ATENGENEZA KOMBINESHI MATATA…


KUREJEA kwa mshambuliaji Mzambia Lazarous Kambole kumemlazimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kutengeneza kombinisheni mpya ya ushambuliaji hatari.

Kambole amerejea uwanjani juzi na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake huko kambini Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambako wameweka kambi.

Mzambia huyo alikuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili akiuguza maumivu ya misuli aliyoyapata kwenye pre-season walipocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Namungo FC huko Avic Town.

Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, amesemakuwa mara baada ya Kambole kurejea uwanjani, kocha ameonekana akiijaribu kombinesheni yake na kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki.

Bosi huyo alisema kuwa kocha huyo ameonekana kumchezesha Kambole namba 9 huku Aziz Ki nyuma yake 10 ambaye amempa jukumu la kumchezesha kwa mipira mizuri ya kufunga wakiwa mazoezini huko Avic Town.

Aliongeza kuwa kocha huyo ameonekana kuvutiwa na Kambole mazoezini kutokana na kiwango bora cha kufunga mabao ambacho amekionyesha akiwa ndani na nje ya 18.

“Tuna jumla ya washambuliaji watatu katika timu, ambao wote anakubali uwezo wao kutokana na umahiri mkubwa wa kufunga mabao walionao uwanjani.

“Hivyo basi anajaribu kutengeneza kombinesheni tofauti za ushambuliaji, mara kadhaa amekuwa akimchezesha Mayele, Makambo wote wakicheza namba 9 lakini nyuma yao anakuwepo Aziz Ki.

“Lakini juzi mara baada ya Kambole kurejea uwanjani na kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake, ameonekana akimchezesha pamoja na Aziz Ki.

“Kwa maana ya Kambole kucheza namba 9 na Aziz Ki 10, kocha huyo anaitengeneza kombinesheni hiyo mpya ya ushambuliaji kwa lengo la kusuka kikosi imara ambacho hakitamtegemea mchezaji mmoja pekee katika timu,” alisema bosi huyo.

Nabi alizungumzia hilo kwa kusema: “Najaribu kutengeneza ushindani wa namba katika timu kwa kila mmoja kupambania namba ili aingie katika kikosi cha kwanza.

“Kama nilivyoongea awali, bado kikosi changu hakijakamilika kwa asilimia mia moja, hivyo najaribu kutengeneza timu itakayokuwa imara na kutengeneza mzunguko wa wachezaji kucheza kwa kupishana kwa lengo la wengine kupumzika, kwani tuna mashindano mengi msimu huu.”

SOMA NA HII  GAMONDI AFANYA KILA KITU MAPEMA SANA