Home Habari za michezo HUU HAPA UKWELI KUHUSU MASTAA YANGA KUPIKIWA CHAKULA MAAMULU CHA USHINDI LEO…WAPIGWA...

HUU HAPA UKWELI KUHUSU MASTAA YANGA KUPIKIWA CHAKULA MAAMULU CHA USHINDI LEO…WAPIGWA MARUFUKU….


Zimesalia saa kadhaa tu kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuikabili Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022-2023, mastaa wa Yanga wameandaliwa msosi maalumu ili kuhakikisha wanatakata leo.

Mbali na kuandaliwa msosi maalumu, nyota hao wa Yanga wametengenezewa mipango ya kuhakikisha wanakuwa na utimamu wa mwili na akili kabla ya mchezo huo wa ngao na mingine ya michuano watakayoshiriki.

Daktari wa Yanga, Dk Shecky Mngazija ameeleza jambo hilo limeanza wiki tatu zilizopita baada ya kikosi cha Yanga kuanza kujiandaa kutetea mataji yake mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC huku ikitarajiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itaanzia raundi ya awali na siku chache kabla ya kuvaana na Simba Kwa Mkapa.

“Kwenye suala la utimamu wa mwili na akili wapo vizuri kwani kabla wachezaji wetu hawaajanza msimu huu mpya tumewafanyia vipimo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete,” alisema Mngazija na kuongeza wamewapangia wachezaji msosi, kutaka wapumzike sambamba na kufanya mazoezi yatakayowafanya wawe fiti kimwili na kiakili ili kuibeba timu hiyo.

Dk Mngazija akafunguka misosi ambao wachezaji wa Yanga wamepangiwa kula kwa kusema; “Wachezaji wanahitaji nguvu kwa asilimia kubwa hivyo tunawapa kipaumbele kwenye vyakula vya wanga kwa 70%, protini 15%, mafuta 10%, madini na vitamini 5%;” alisema Ngazija na kuongeza;

“Tunapendelea kuwapa vyakula kama mihogo, mahindi kwa kuwa vina wanga mwingi, matunda, maji na mboga za majani kwa wingi kwa kuwa tunaamini afya bora ndio mtaji wa wachezaji kwa kufikisha malengo ya timu.”

Akizungumzia aina ya viwanji, Dk Mngazija alisema; “Wachezaji wetu mbali na maji, kinywaji pekee tunachowashauri kutumia na tunawapatia kwa wingi ni juisi ya matunda asilia na hatuweki sukari yoyote kwa kuwa sukari haturuhusu kutumia pasipo kuchemshwa jikoni.”

Dk Mngazija alisema kama daktari wa timu anashirikiana na wataalamu wao wa misosi na mpishi ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa fiti na kufafanua zaidi; “Katika vyakula ambavyo tunazuia kwa wingi ni matumizi makubwa ya protini kwa wachezaji wetu kwani vikitumika kwa wingi inachangia kuongezeka kwa mafuta na uzito hivyo inaweza kumnenepesha mchezaji.

SOMA NA HII  BREAKING:YANGA YAMTAMBULISHA KIPA MWINGINE TENA

“Pia vyakula vya sukari tunatoa kwa kipimo maalumu kwa wachezaji wetu na hii ni hutokana na athari za matumizi makuwa ya sukari yanayochangia kuongezeka kwa uzito na uzito unapozidi ni tishio kwa wachezaji na matumizi ya chumvi ni kitu tuchonazingatia.”

Dk Mngazija aliongeza kuhusu vinywaji walivyozuia wachezaji kutumia kwa kusema; “Pombe ni moja ya vitu ambavyo haturuhusu wachezaji wetu kutumia kwa kuwa pombe hukausha maji mwilini kwa kiwango kikubwa. Unapokunywa pombe lita moja unapokwenda haja ndogo unapoteza lita moja na robo ya maji mwilini na maji ni muhimu kwa mchezaji.”

“Vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) na soda haturuhusu kabisa kwa kuwa soda zinabeba sukari nyingi sana ambazo ni hatari kwa afya zao hasa mapigo ya moyo na uzito,” alisema Dk Mngazija na kuongeza;

“Unajua mchezaji akipata mazoezi makali sana husababisha kupata majeraha ya mara kwa mara au hushindwa kucheza kwa kiwango chake, tumekuwa tukishirikiana na watu wa kitengo hicho ili uwepo usawa kwa kila jambo. Kitu kingine kinachowajenga wachezaji wetu ni muda wao wa kupumzisha mwili na akili, tunawapa mapumziko ya kutosha.”