Home Habari za michezo KAMA ULIKUWA HUJUI….HII HAPA REKODI NYINGINE YA KIBABE YANGA WALIYOIWEKA KWA KUIFUNGA...

KAMA ULIKUWA HUJUI….HII HAPA REKODI NYINGINE YA KIBABE YANGA WALIYOIWEKA KWA KUIFUNGA SIMBA JUZI…


USISHANGAZWE na matokeo ya dabi ya Kariakoo ya Agosti 13, 2022 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii, Yanga ilipindua meza na kuifunga Simba mabao 2-1.

Ni baada ya Simba kutangulia kwa bao la dakika 16 la Pape Ousmane Sakho na Fiston Mayele kuchomoa dakika ya 50 kisha kupigilia msumari dakika ya 81. Hii siyo mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kufanya ‘comeback’ au kupindu meza.

Historia inaonyesha Yanga imepindua meza mara saba mbele ya watani zao hao, huku Simba ikifanya hivyo mara sita.

Hizi hapa mechi ambazo timu hizo zimeonyeshana ubabe wa kupindua meza tangu 1966.

Juni 3, 1966 katika Uwanja wa Taifa, (sasa Uwanja wa Uhuru) Simba ikiwa inatumia jina la Sunderland ilitangulia kupata bao  mapema dakika ya 24 lililofungwa na Mustafa Choteka. Lakini Yanga wakati huo ikiitwa Young Africans ilisawazisha kupitia kwa Abdulrahaman Lukonge  dakika 54. Kama haitoshi Yanga ikafunga bao la pili kupitia Andrew Tematema na Emmanuel Makaidi akahitimisha la tatu dakika ya 83. Sunderland ilipata bao la pili kupitia kwa Haji Lesso dakika ya 86 lakini halikubadili matokeo ya ushindi.

Agosti 10, 1974 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Simba ilitangulia kufunga dakika ya 16 lililowekwa kimiani na Adam Sabu, lakini Yanga ilipindua meza dakika za mwishoni kwa bao la Gibson Sembuli dakika 87 na Sunday Manara 90+7.

Aprili 16, 1983 beki wa Simba, Mussa Kihwelo (kaka yake na Jamhuri Kihwelo) aliifungia Simba bao dakika ya 14,  Yanga ilipindua matokeo kwa kufunga mabao  matatu kupitia kwa Boniface Mkwasa dakika 21, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ dakika ya 38 na Omary Hussein dakika 84.

Agosti 23, 1986 Yanga ilitangulia kwa bao la Omary Hussein dakika ya tano, lakini Simba ikapindua meza kupitia Edward Chumila dakika 9 na Malota Soma dakika ya 51. Oktoba 4, 1995 Mohammed Hussein aliifungia Yanga bao la dakika 40 na Simba ilichomoa kupitia Said Mwamba na Mchunga Bakary akafunga bao la ushindi.

SOMA NA HII  KRAMO NNJE TENA SIMBA....AL AHLY WAINGIZA MASTAA WAPYA MECHI YA KESHO....

Mei Mosi 1999, Juma Amir aliifungia Simba bao la dakika 12, lakini Yanga ikapindua meza kibabe kwa mabao ya Idd Moshi dakika ya 59, Kalimangonga Ongala dakika ya 64 na Salvatory Edward  dakika ya 70.

Juni 25, 2000 Idd Moshi aliipatia Yanga bao la dakika ya nne, lakini Steven Mapunda wa Simba alifunga mara mbili katika dakika 59 na 72 (kama alivyofanya Mayele Jumamosi iliyopita).

Agosti 7, 2004 raia wa DR-Congo, Pitchou Kongo aliifungia Yanga bao dakika ya 48 lakini Shabani Kisiga alisawazisha dakika 64 na Ulimboka Mwakingwe kufunga la ushindi dakika 76.

Aprili 17, 2005, mjini Morogoro, Aaron Nyanda wa Yanga aliifungia bao la kuongoza dakika ya 39, ila Simba ilipundua meza kwa mabao ya Nurdin Bakari dakika 44 na Athumani Machupa dakika 64.

Februari 25, 2017 Simon Msuva wa Yanga aliifungia bao la penalti dakika ya tano na Simba ikapindua meza dakika ya 66 kupitia Laudit Mavugo na Shiza Kichuya dakika 81.

Februari 17, 2001 katika mchezo wa Ngao ya Jamii kama wa Jumamosi iliyopita Simba ilipata bao la kuongoza dakika 43 lililofungwa na Steven Mapunda na Yanga ikapindua meza kupitia kwa Edibily Jonas Lunyamila dakika 47 na Ally Yussuf dakika 80.

Novemba 15, 2000 katika Kombe la FAT (sasa Azam Sports Federation), Ally Yussufu aliyehamia Simba aliifungia timu yake bao la dakika ya 37 na Yanga kupindua meza kupitia kwa Aziz Hunter dakika ya 40 na Vincent Tendwa.