Home Habari za michezo KUHUSU TAMASHA GANI KATI YA SIMBA DAY NA SIKU YA WANANCHI LIPI...

KUHUSU TAMASHA GANI KATI YA SIMBA DAY NA SIKU YA WANANCHI LIPI LILIKUWA BORA…UKWELI WA TAKWIMU HUU HAPA…


Hatimaye msimu mpya wa Ligi Kuu Bara umefunguliwa rasmi jumamosi iliyopita kwa mechi ya Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga. Matokeo ndio kama mlivyosikia. Wa kununa na wanune.

Lakini habari njema zaidi ni kufanyika kwa matamasha ya Siku ya Wananchi na Simba Day wiki moja iliyopita. Hakika Tanzania imeendelea kuwa katika sayari ya peke yake.

Rafiki yangu mmoja kutoka Uganda ameniambia hajawahi kuona vitu kama hivyo sehemu nyingine Afrika. Ameshangazwa sana na utaratibu wa Simba na Yanga kutambulisha wachezaji pamoja na benchi la ufundi. Ameshangazwa zaidi na umati uliojitokeza kwa Mkapa Inapandeza sana.

Hata hivyo baada ya matamasha hayo mambo mengi yameibuka. La kwanza ni mwitikio tofauti wa mashabiki wa Simba na Yanga. Ni wazi kuwa Simba walifurika zaidi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Uwanja ulijaa pomoni. Hakukuwa hata na sehemu ya kusimama. Kulijaa mpaka kwenye ngazi na bomba za kutenganisha majukwaa. Watu walikuwa wengi kama sisimizi waliokutana na kiporo. Inavutia mno.

Kwanini Simba walifurika zaidi? Hili ni swali ambalo watu wengi hawataki kulizungumza.

Kwanza, Simba imefanya tamasha hilo kwa miaka 14 sasa. Ndio waasisi wa matamasha haya ya soka nchini. Walianza kwa mwendo wa kinyonga, wakaendelea kuufanya kuwa utamaduni kila mwaka. Sasa ni wazi kuwa Simba imefika katika kilele cha mafanikio yake.

Pili, Simba iliweka kiingilio rafiki katika tamasha lake. Simba inafahamu kuwa lengo la Simba Day siyo kuingiza kipato, bali ni kutambulisha timu. Kujenga brandi ya klabu pamoja na kuonyesha ukubwa wake.

Tatu, ni kutoa nafasi kwa wadhamini na wadau wengine kuona ukubwa wa Simba. Hili ndio lengo halisi. Ukishafanikiwa kuonyesha ukubwa wako, unapata dili za pesa baadaye.

Hii ndiyo sababu Simba sasa ina wadhamini tisa tofauti. Hii ndiyo sababu Simba imepata mkataba mpya wa udhamini wenye thamani kubwa zaidi ya timu yoyote Afrika Mashariki na Kati. Ni kwasababu ya matukio kama haya.

Ni kama vile Simba hufanya katika michuano ya Afrika. Mechi zote kali kwa Mkapa Simba huweka kiingilio cha chini Sh. 3000 tu. Mashabiki wanafurika kuipa sapoti timu yao. Mzuka unakuwa mkubwa kwa Mkapa, na mwisho wa siku timu zote zinapaona kuwa sehemu ngumu kucheza.

SOMA NA HII  ISHU YA SIMBA NA MGUNGA BADO PASUA KICHWA...MWENYEWE AWAWEKEA NGUMU MABOSI...

Ndio njia hii imeifanya Simba kuwa maarufu huko Afrika, lakini wamefanikiwa kwa kujali uwezo wa mashabiki wa soka nchini. Watu wengi wanaopenda soka nchini hawana uwezo mkubwa wa kifedha. Hivyo kuweka kiingilio kikubwa ni kuwanyima fursa ya kufurahia timu yao.

Hapa ndipo Yanga walipokwama. Pamoja na mafanikio makubwa ya Yanga msimu uliopita. Pamoja na usajili wa wachezaji wakubwa kama Stephane Aziz Ki. Kwanini Yanga ilishindwa kuujaza Uwanja wa Mkapa?

Ni kwa sababu walitumia tamasha lao kama sehemu ya kupata kipato zaidi, na siyo kuonyesha ukubwa wao. Hawakutumia Siku ya Wananchi kama sehemu ya kuwapa wadhamini fursa kubwa ya kuonekana, bali sehemu ya kupata pesa. Yawezekana wamefanikiwa katika malengo yao, lakini katika mioyo ya mashabiki wameacha majonzi.

Simba waliwahi kufanya kosa kama hilo miaka miwili nyuma. Waliamini kwamba timu yao imekuwa kubwa sana. Wakaweka viingilio visivyo rafiki. Wakamchukua na Diamond Platinumz akashuka na Chopa pale Lupaso. Nini kilitokea?

Uwanja ulijaa mapengo kama kinywa cha mzee. Yaani Simba na Diamond wakashindwa kuujaza Uwanja wa Mkapa. Ilichekesha sana. Kwanini? Kwa sababu hawakuweka viingilio rafiki.

Simba hawatakaa warudie kosa hilo tena. Kosa ambalo Yanga wamelifanya msimu huu na kushusha brandi ya timu yao.