KUNA asilimia kubwa beki wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akajiunga na Dodoma Jiji kwa mkopo, kutokana na nafasi finyu ya kucheza ndani ya kikosi cha Wanajangwani.
Awali Ninja ilikuwa atolewe kwa mkopo Geita Gold, iliyoshindwa kutimiza moja ya kipengele ilichotakiwa ikifanye, ambacho Dodoma Jiji imekiweza, hivyo ndani ya wiki hii Ninja anaweza akaondoka Yanga.
Taarifa ya chanzo cha ndani inasema; “Dodoma kwa asilimia kubwa imetimiza masharti ya kumchukua kwa mkopo Ninja, ndani ya wiki hii anaweza akajiunga nao.”
“Ninja ni beki mzuri anahitaji kupata nafasi ya kucheza ili kurejea kwenye makali yake, baada ya kusumbuliwa na majeraha kwa muda mrefu, ambayo yalimfanya akae nje kwa muda mrefu.”
Chanzo hicho kilisema tayari kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi alishatengeneza pacha kati ya Shaban Djuma na Dickson Job, wakati mwingine wanacheza Job na Bakari Mwamnyeto ambao wanaonyesha kiwango cha juu.
“Ninja akitoka akapata uzoefu wa mechi utamrejesha kwenye kujiamini na akafanya kazi yake kama mwanzo, ndio maana Yanga ilimuongeza mkataba ikitambua kipaji chake,” kilisema chanzo hicho.