Rais wa Yanga, injinia Hersi Said amesema anafahamu ligi ni ngumu msimu huu lakini wana ubora mkubwa tofauti na timu zingine na sasa gari ni kama limewaka ndani na nje.
Hersi amesema kuwa wakiziangalia timu zingine kisha kulinganisha na kikosi chao ni kwamba Yanga haikupoteza uti wa mgongo wa kikosi chao kwa kuwabakisha mastaa wao wote waliofanya vizuri msimu uliopita.
“Tathimini ambayo tumeifanya kama uongozi ni kwamba bado tuna timu bora kushinda timu yoyote na hii kuna mambo ambayo tumeyafanya mpaka ubora huo ukawa hivyo, hatukufanya makosa ya kuwaruhusu wachezaji wetu bora ambao walitupa mafanikio makubwa.
“Ule uti wa mgongo wa kikosi chetu upo salama hii ni tofauti kubwa na timu zingine na hao tuliowabakiza bado wanashindana kutupa ubora zaidi,”alitamba.
Alisema hatua ya pili ni ongezeko la mastaa wao wapya ambao licha ya ubora wao mkubwa wamejikuta kuja kushindana na wenzao waliowakuta ambao ushindani huo umeongeza thamani kubwa kwenye kikosi hicho.
“Ukichana na hilo angalieni pia ongezeko la wachezaji wapya ambao tuliwasajili dirisha hili Lomalisa (Joyce),Bigirimana (Gael) watu wameanza kuona makali yake taratibu,Aziz KI Stephane kila mtu ameona thamani yake, pia nenda kwa Morrison nadhani watu wanaona jinsi alivyorudi na akili mpya tofauti na walivyodhani.”
“Kuna Kambole (Lazarous) watu hawajamuona lakini akishakuwa sawa watakuja kujua ubora wake kama haitoshi tumemwongeza na Kisinda (Tuisila) kuja kuongeza ile kasi yake utaona hawa wote ni watu bora ambao makocha wetu waliwahitaji.”
Hersi aliongeza kuwa sababu ya tatu ni aina ya benchi lao la ufundi likiongozwa na kocha mkuu wao Nasreddine Nabi na wasaidizi wake ambao kwa pamoja wamezidisha ugumu wa kikosi chao kuwa bora.
“Tuna kocha mwenye ubora mkubwa na leseni kubwa ya UEFA diploma pro (Nabi) lakini pia kuna mwingine mwenye leseni A ya CAF(Cedric Kaze) ukiongeza na wasaidizi wao wengine kama Milton ambaye naye leseni yake ni kubwa utaona jinsi tulivyokamilika na hawa wote wameendelea kuthaminika na kutuoa ubora katika kazi yao.
“Sio kila timu imekuwa na ubora huo wapo ambao wameshafukuzwa na kuanza upya lakini sisi Yanga tumebaki na utulivu mkubwa hii ni jinsi tunavyojitofautisha na wengine kiubora kwahiyo haya yote tunayapima na kuona tuna kila sababu ya kuzidi kuendelea kushikilia mataji haya.”