Home Habari za michezo SIKU KADHAA TOKA ASEPE MSIMBAZI …MHILU AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA MAZITO KUHUSU SIMBA NA...

SIKU KADHAA TOKA ASEPE MSIMBAZI …MHILU AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA MAZITO KUHUSU SIMBA NA MO DEWJ…


KUNA malalamiko mengi sana kwa wachezaji wazawa wanaposhindwa kufanya vizuri kwenye timu za Simba na Yanga.

Je, kuna mtu ameshakaa nao na kuwauliza kitu gani wanachokipitia pindi wanapofika katika timu hizo?

Majibu hayo anayo winga wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu aliyerudi katika timu hiyo akitokea Simba.

Mhilu alitoka Kagera Sugar Msimu wa 2020/21 akiwa kinara wa timu akiwa na mabao tisa. Kipaji chake kiliwavutia Simba na kumsajili. Hiihaikuwa mara yake ya kwanza kufunga mabao mengi, kwa sababu msimu wa (2019/20) alimaliza na mabao 13.

Kwa nini hakufikisha hata mabao matano akiwa Simba? Katika mahojiano baina yake na gazeti la  Mwanaspoti, Mhilu anafunguka vitu alivyopitia ndani ya mwaka mmoja akiwa Simba alikosaini mkataba wa miaka mitatu.

“Nimejifunza mengi, wachezaji tunahitaji watu wa kutuongoza pale tunapokuwa na changamoto tunazozipitia, kuna wakati mwingine tunasemwa vibaya bila ya wengine kutojua kinachotuumiza,” anaanza kufunguka.

TATIZO HILI HAPA

Ni ndoto ya kila mchezaji kuzichezea Simba na Yanga, lakini kabla ya kupata bahati hiyo, wachezaji wanatakiwa kujiandaa kiakili jinsi ya kukabiliana na ushindani pindi wanapojiunga na Simba naYanga.

Hali hiyo itafanya vipaji vyao kufika mbali.

Simba na Yanga zinapendwa na watu wengi kwa sababu zinapata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF mara nyingi, zipo vizuri kiuchumi na ni matajiri wa mashabiki ambao wanaweza wakamfanya mchezaji thamani yake ipande ama ishuke kabisa.

Mhilu ni shuhuda wa jambo hilo, alitoka Kagera Sugar akiwa na kiwango cha juu, baada ya kutua Msimbazi alikiona cha mtema kuni, matarajio yake ya kuanza kikosi cha kwanza yaliyeyuka baada ya kukutana na ugumu ndani ya kikosi hicho.

“Simba na Yanga zinahitaji viwango, hazina muda wa kujua mchezaji unapitia kipindi gani. Unapewa kila kitu unachostahili, kile wanachokupa wanataka ukilipie uwanjani. Lakini sisi ni binadamu kuna wakati tunapitia mazito ambayo yanaweza yakatutoa kwenye mstari, mbaya tunakosa msaada wa kimawazo,” anasema Mhilu.

“Simba ukipewa mechi moja ukacheza chini ya kiwango basi utakomaa na benchi kwani hakuna wa kukuuliza una changamoto gani. Kuna wakati mchezaji anatamani mtu sahihi wa kumuongoza pindi moyo unapopitia magumu lakini anashindwa, hilo ndilo linalowakumba vijana wengi katika timu hizo.”

Mhilu anaongeza “Sio kweli kwamba kila mchezaji anayepita kwenye timu hizo anakuwa hana uwezo au anashindwa kuendana na kasi ya ushindani wa namba bali kuna changamoto nyingi zinazosababisha kutokuwa vizuri.”

Anasema ili wachezaji wanaopita kwenye timu hizo wafanye vizuri wanatakiwa kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuonyesha kile kilichopo kwenye miguu yao na sio kukatishwa tamaa wanapokosea mara moja.

“Kuna umuhimu wa timu hizo kutafuta wanasaikolojia wa kukaa na wachezaji hasa timu inapofungwa kwenye ili wafahamu wana shida gani na kuwajenga kiakili.

“Sisi ni binadamu pia tunatakiwa kusikilizwa na kufanyiwa tathimini kabla ya kutuondoa kwenye timu zao kwani mchezaji hawezi kupimwa kwa mechi moja na ili kumjenga akiharibu mpe dakika nyingine kesho ili arekebishe makosa yake.

“Mchezaji leo anaweza kucheza vibaya na kesho akawa mtu mwingine kabisa, anaweza akacheza vibaya kutokana na changamoto zinazomsumbua kwenye maisha yake binafsi labda kaumizwa kimapenzi au familia yake ina shida kukiwa na mwanasaikolojia anaweza kukaa naye na kumuweka sawa.”

KUTUA SIMBA NI MIPANGO

“Kocha Diddie Gomes aliniona nikiwa Kagera Sugar baada ya kucheza nao na kuniambia kuwa mimi ni mchezaji mzuri natakiwa kuongeza juhudi ili niweze kufikia malengo akaondoka kisha siku nyingine nikafuatwa na msaidizi wake, Seleman Matola ambaye alinishawishi nijiunge nao,” anasema na kuongeza;

“Baada ya kuniambia hivyo nilimwambia kuwa nina mkataba hivyo natakiwa kufanya mazungumzo na uongozi ila baada ya hapo ukimya ukatawala nikawa naendelea na maisha yangu ndani ya Kagera nakumbuka kilikuwa ni kipindi cha dirisha dogo,” anasema.

Mhilu anasema anakumbuka akiwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 (U-23) ambapo walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Cecafa U-23 baada ya kuifunga kwa mikwaju ya penati 6-5 Burundi katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Bahir Dar Ethiopia Julai 30, mwaka jana uongozi wa Simba ulirudi tena.

“Nilikuwa miongoni mwa vijana walioisaidia timu hiyo kutwaa taji ndipo vita mpya ya kunasa saini yangu iliibuka kimyakimya na kufanikisha kuninasa kwa mkataba wa miaka mitatu nikitumikia mmoja na sasa nipo kwa mkopo wa mwaka mmoja Kagera Sugar,” anasema.

KIPAO AMPA KITANDA

Utani kwenye timu haukosekani kwani siku chache baada ya Mhilu kuamua kurudi kwenye timu yake ya zamani alipokewa kwa utani na baadhi ya wachezaji wenzake waliokuwa wanaishi pamoja kabla hajaondoka ndani ya timu hiyo na kwenda kujaribu maisha yake Simba.

“Nilipokuwa Kagera kabla ya kwenda Simba nilikuwa naishi nyumba moja na mdogo wangu Dickson Mhilu, Said Kipao ambaye ni kama alijua kama nitarudi tena, alinipokea kwa kuniambia karibu sana kitanda chako kilikumisi hakuna mtu alipewa nafasi ya kukitumia,” anasema.

SOMA NA HII  KOCHA WA SIMBA SVEN KURUDI BONGO

“Akakisogelea kitanda na kuniambia karibu nyumbani hiki kitanda chako hakijatumiwa na mtu yeyote kinakuwa kimekumisi hakijapata mtu kwa sababu kilijua utarudi hivyo maisha mengine yaendelee.”

MPOLE KAWAPA ELIMU

“Siku zote imekuwa ikiaminika kinara wa mabao anatakiwa kutoka Simba, Yanga na Azam FC kutokana na usajili wanaoufanya unaokuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na uwezo mkubwa wa kucheza wakitoka mataifa mbalimbali na kuchanganya na wazawa lakini George Mpole (Geita Gold) ambaye alikuwa kinara msimu ulioisha akifunga mabao 17 ametupa somo” anasema na kuongeza;

“Mpole katuaminisha kuwa kiatu kinaweza kutoka nje ya timu hizo. Natumia nafasi hii kumpongeza ametuamsha usingizini ametufanya na sisi tuongeze juhudi ya kupambana ili kuweza kufikia malengo aliyoyafikia yeye msimu uliopita.”

NYONI AMPA NENO

“Kipindi nilipotua Simba rafiki yangu alikuwa ni Erasto Nyoni kwa sababu tunakaa karibu, hivyo mara nyingi nilikuwa napata lifti kwenye gari yake kwa ajili ya kwenda mazoezini au kambini alikuwa mtu mzuri sana kwangu akinisisitiza kufanya kazi kwa kujituma zaidi,” anasema na kuongeza;

“Mara nyingi alikuwa ananisisitiza kuwa mpira sio kitu cha kukitegemea sana kinaweza kunipoteza muda wakati wowote lakini kwa kuwa nimeamua kutua Simba nifanye kile kilichonipeleka pale na kujitahidi kuwekeza kwenye mambo mengine na sio kuuamini mpira kama kazi yangu ya maisha,” anasema Mhilu.

“Kauli yake ambayo sitakaa nikaisahau ni hii ‘Hapa umekuja mwenyewe jipambanie mwenyewe hakuna mtu atakayekusaidia unatakiwa kujisaidia hii itaishi sana kwenye maisha yangu ni kweli nilienda mwenyewe na kuondoka mwenyewe.”

Anaongeza mbali na Nyoni pia alikuwa na ukaribu n Jimmyson Mwanuke, Peter Banda na Pape Sakho pamoja na urafiki aliokuwa nao hajaweza kuondoka nao kaondoka yeye kama yeye hivyo kauli ya Nyoni inaishi kwenye kichwa chake.

ISHU KABWE WARRIORS

“Uongozi wa timu ya Kabwe Warriors ulituma ofa Simba kuniomba kwa mkopo na wakanishirikisha niongee na meneja wangu kuhusiana na ofa iliyokuja mezani. Nilifanya hivyo wakati mazungumzo kati yetu na uongozi wa Kabwe yakiendelea Simba walinitoa kwenye usajili wa wachezaji wao,” anasema.

“Baada ya makubaliano kwenda tofauti na Kabwe nilirudi tena Simba kuwaambia kuwa ofa waliyoweka mezani ni ndogo, hivyo kujiunga na timu hiyo kwa mkopo haiwezekani ndipo waliponiambia kuwa wao wamenitoa kwenye usajili nitafute mwenyewe timu ambayo itaweza kunihudumia kwa kila kitu.”

Mhilu anasema dau la Kabwe lilikuwa dogo kwani lilikuwa limeongezeka kwa asilimia ndogo ambayo kodi ya Zambia ikikatwa hawezi kuambulia chochote, hivyo hakuona umuhimu wa kwenda kwa sababu angekuwa anatumia nguvu bila kupata chochote.

“Baada ya hapo ndipo tulipokaa meza moja na viongozi wa Kagera na kusaini mkataba mpya ambao ndio nitakaoutumikia msimu huu ambao tayari umeanza na nimepata nafasi ya kucheza mechi moja.”

MO DEWJI ALIMKARIBISHA SIMBA

Mhilu anafunguka ziadi kuhusu usajili wake ambao ulikuwa gumzo na kuwashtua watu wengi.

“Usajili wangu uliwashtua wengi kutokana na namna ulivyofanywa kwa siri kubwa tofauti na usajili mwingine wowote kwani baada ya kutua kutoka Burundi nilikamilisha usajili chini ya mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewj ‘MO’ ambaye aliniambia anafurahi nimekubali kutua ndani ya timu hiyo,” anasema na kuongeza;

“Aliniambia yeye ni muumini wa wachezaji vijana na Simba ndio sehemu sahihi kwangu kwa sababu imekuwa ikitoa nafasi ya kukuza vijana na kunikaribisha ndani ya timu akinitakia kila la kheri kwa kuniambia kuwa natakiwa kufanya kazi kwa umakini na usikivu mkubwa ili niweze kufikia mafanikio.”

Mhilu anasema MO alimwambia kuwa afanye kilichompeleka Simba hatakiwi kujichanganya na vitu vingine kutokana na umri wake ni tunu kwa taifa kwa miaka ya baadaye.

PABLO AMUONDOA SIMBA

“Pamoja na kufuatwa na (kocha Selemani) Matola huku dili likikamilishwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori ambaye alimalizana na uongozi wa Kagera Sugar kwa ushawishi lakini Kocha Diddie Gomes ndiye aliyekuwa amekubaliana na kipaji changu na kuuomba uongozi unisajili,” anasema.

“Chini yake akiwa kocha mkuu nilipata nafasi ya kucheza mara kwa mara na alikuwa kocha ambaye alikuwa ananizingatia kwenye kila mchezo.

“Nilipokosea ananiambia lakini naomba nikiri kwamba baada ya kocha huyo kuonyeshwa mlango wa kutokea ndio ukawa mwanzo wangu wa kukosa nafasi ya kucheza.”

Mhilu anasema alipokuja Kocha Pablo Franco hakumthamini kama alivyokuwa akithaminiwa na Gomes.

Mchezaji huyo anasema kila kocha ana aina ya wachezaji anaowataka na ujio wa Pablo haukuwa mzuri kwani hakuwa chaguo lake hadi anaondoka Simba hakuna kocha aliyemthamani tena.