Home Habari za michezo TFF YAMBAKISHA ONYANGO SIMBA…SAKATA LA KISINDA LAZUA JAMBO JIPYA…KAMATI YAMTUPA DIRISHA DOGO…

TFF YAMBAKISHA ONYANGO SIMBA…SAKATA LA KISINDA LAZUA JAMBO JIPYA…KAMATI YAMTUPA DIRISHA DOGO…


Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imekata mzizi wa fitina kwa kuuzuia usajili wa winga aliyerejea Yanga, huku ikimrudisha beki Joash Onyango kuendelea kuitumikia Simba aliyotaka imteme ili ajiunge timu nyingine.

Kamati hiyo ilikutana juzi jijini Dar es Salaam kupitia mapingamizi ya sajili za wachezaji wa klabu mbalimbali pamoja na kesi kadhaa ikiwamo ya Onyango aliyekuwa akiomba kuachwa na Simba na taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ni kwamba Yanga imekwama kumtumia Kisinda katika kipindi hiki na sasa itasubiri hadi dirisha dogo, huku Simba ikiruhusiwa kuendelea kumtumia beki wake Onyango.

Yanga iliipeleka pingamizi la Kisinda kutaka atumike kutokana na kuwahi dirisha kubwa la usajili kabla halijafungwa Agosti 31 ikimsajili kwa mkopo kutoka RS Berkane ya Morocco, lakini imekuwa tofauti kutokana na jina la mchezaji huyo kushindwa kupenya kwenye usajili kutokana na klabu hiyo kuwa tayari imeshakamilisha majina 12 ya wachezaji wa kigeni kama sheria inavyotaka.

Yanga ilikuwa imeomba kumchomoa mshambuliaji kutoka Zambia, Lazarous Kambole ili imuingize Kisinda, lakini ilipokea barua kutoka TFF ikisainiwa na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao ikimzuia kwa maelezo tayari ilishakamilisha idadi ya wachezaji wa kigeni kikanuni.

Onyango naye akipeleka barua Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) akiomba kutengua mkataba wake na Simba kwa kile kilichoelezwea kwamba haoni kesho yake kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Baada ya kamati kukutana Ijumaa imefahamika kuwa Onyango ni mchezaji halali wa Simba na ataendelea kuitumikia timu hiyo huku Kisinda ikisemekana kuwa anatakiwa kusubiri hadi dirisha dogo.

Kisinda ambaye amerejea Jangwani akitokea RS Berkane ya Morocco na kutua Yanga kwa mkopo atatakiwa kusubiri dirisha dogo la usajili ili aweze kuwa mmoja wa wachezaji watakaoweza kuichezea timu hiyo kutokana na usajili wake kushindwa kufanyika dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 31 na Klabu zote ziliruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12.

“Kweli tulikaa kikao Ijumaa na kupitia mapingamizi yaliyofika mezani kwetu na kuhusiana na wachezaji uliowataja Onyango ametakiwa kuendelea kuitumikia Simba huku Onyango akitakiwa kusubiri dirisha lingine la usajili baada ya usajili wake kushindwa kukamilika,”kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kamati.

SOMA NA HII  AHMED ALLY AMTABIRIA BALEKE MVUA YA MAGOLI

Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu  alisema taasisi ina utaratibu wake muda ukifika watatolea ufafanuzi mambo hayo.

“Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kuhusiana na yaliojili kwenye kamati hiyo kwasababu TFF inautaratibu wake wa kutoa taarifa hivyo itatolea ufafanuzi suala hilo muda ukifika,” alisema Kidifu.