Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU….PAMOJA NA YOTE YANAYOENDELEA SIMBA…SIO BURE KUNA MAHALI HAPAKO SAWA…/MwanaSpoti.

UKWELI MCHUNGU….PAMOJA NA YOTE YANAYOENDELEA SIMBA…SIO BURE KUNA MAHALI HAPAKO SAWA…/MwanaSpoti.


ACHANA na taarifa za vyeti na leseni za CAF. Achana na taarifa za Simba kudaiwa kuazima kocha na Coastal Union kukanusha.

Achana na zile kelele za mashabiki wa Simba kumkataa Matola pale kwa Mkapa. Achana na taarifa za Kocha Zoran Maki kuachana na Simba asubuhi na kutangazwa na timu ya Ligi Kuu Misri mchana.

Achana na mambo yote unayosikia kwenye soka letu. Ukweli ni kwamba pale Simba kuna kitu hakiko sawa.

Sijui kama una fikra sawa na zangu. Sijui kama una mtazamo sawa na wangu. Ila ukweli pale Simba kuna shida. Kuna tatizo kubwa sana.

Tuanze na hili la Kocha Zoran kuondoka Simba asubuhi na kutangazwa na Al Ittihad ya Misri mchana. Hii inachekesha sana.

Taarifa ya Simba ilisema ameondoka baada ya pande zote mbili kuridhia kusitisha mkataba wake. Ila katika uhalisia haiko hivyo.

Uhalisia ni Zoran alipata kazi nyingine yenye masilahi zaidi pale Misri. Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kocha huyo alianza kuzungumza na Al Ittihad muda mrefu.

Hii inamaanisha Simba ilikiwa ikifahamu hili. Viongozi walishaona dalili za Zoran kuondoka mapema. Sitaki kuamini kama hakuwapa taarifa za ofa yake hiyo.

Lakini taarifa ya Simba ilitoka kana kwamba wao ndio wameachana na kocha Zoran. Hawakukiri kama amepata ofa nyingine. Kwa nini? Wanafahamu wenyewe.

Kituko zaidi ni kama Simba walifahamu kocha huyo anaondoka, kwa nini hawakujiandaa mapema? Kwa nini na walifahamu kama mechi za Kimataifa zipo karibu?

Nini kimetokea sasa? Wamekwenda kumkodi Juma Mgunda pale Coastal Union. Inachekesha sana.

Siyo kwamba Mgunda ni kocha mbaya, hapana. Ila hii ni mara ya kwanza kwa Juma Mgunda kufundisha timu katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Yes, ni mara ya kwanza.

Ni kweli amewahi kufundisha timu ya Taifa kama kocha msaidizi, lakini huku kwenye klabu hajawahi. Hii ina maana anaanzia hapo Simba.

Kwa Simba hii inayojinasibu inataka kufika nusu fainali Afrika, kweli ndio kwa kocha wa majaribio? Siyo kweli. Kuna jambo tunaongopewa hapa.

SOMA NA HII  YANGA WAIKIMBIZA SIMBA KIMATAIFA...REKODI MPYA ZAIPAISHA ANGA ZA WAARABU...

Kuna mtu hafanyi kazi yake vyema pale Simba. Pengine kuna mtu anataka kuhodhi kazi zote peke yake. Lakini ukweli, kuna jambo haliko sawa.

Mwaka jana Simba ilikumbana na changamoto inayofanana na hii. Iligundua dakika za mwisho kocha Mkuu, Didier Gomes hana vyeti vinavyomruhusu kukaa kwenye benchi katika mechi za CAF.

Nini kilitokea? Gomes akiwa jukwaani alishuhudia Simba ikiondoshwa na Jwaneng Galaxy pale kwa Mkapa. Aliishia kupiga simu zisizo na tija. Simba ikalitia aibu taifa.

Ina maana hawakujifunza jambo? Hili la kumkodi Mgunda dakika za mwisho linafikirisha. Ni ishara Simba katika mipango yao hawako thabiti sana.

Au pengine Simba wanajua namna wanavyoshinda mechi zao hivyo hawana sana ulazima wa kuwa na benchi la ufundi imara sana. Pengine.

Lakini ukweli ni kwamba Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na timu yake wanapaswa kujitathmini. Kuna namna hawazitendei haki nafasi zao.