Home Habari za michezo TIMUA TIMUA NA HAMAHAMA YA MAKOCHA SIMBA….HAWA HAPA MAKOCHA 5 PEKEE WALIOVUMILIWA...

TIMUA TIMUA NA HAMAHAMA YA MAKOCHA SIMBA….HAWA HAPA MAKOCHA 5 PEKEE WALIOVUMILIWA MSIMBAZI…


Simba imeachana na Kocha Zoran Maki akiwa amekaa klabuni hapo kwa siku 67 tangu alipoajiriwa rasmi Julai 1 na kufutwa kazi Septemba 6 mwaka huu.

Zoran ameachana na Simba akiwa ameiongoza kwenye mechi tatu za mashindano – Ngao ya Jamii na kucharazwa mabao 2-1 na Yanga kisha kushinda mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold na kushinda 3-0 na Kagera Sugar iliyowacharaza 2-0.

Mbali na mechi hizo za mashindano, Kocha Zoran ameiongoza Simba kwenye mechi kadhaa za kirafiki za kimataifa zikiwamo nne wakati Simba ikiwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya nchini Misri na miwili iliyocheza Sudan katika mechi maalumu.

Mechi dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na Al Hilal ya Sudan kisha kumalizana na AS Arta Solar 7 ya Djibouti ndipo timu ilipokuwa ikijiandaa kwa mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, mabosi wa Msimbaz wakatangaza kuachana naye baada ya kocha huyo kupata dili nono nchini Misri katika Klabu ya Al Itihad Alexandriea.

Zoran alikuwa ni kocha wa 24 kuinoa Simba tangu mwaka 2001 ikiwa na maana kwamba kwa miaka 21 Simba imekuwa na wastani wa kuwa na kocha kila baada ya mwaka, huku kocha huyo akiwa ni kati ya makocha waliodumu kwa muda mfupi ndani ya timu hiyo.

Rekodi zinaonyesha katika makocha hao 24 ni Mkenya James Siang’a ndiye kocha aliyedumu kwa muda mrefu tangu kipindi hicho hadi leo, akiinoa timu hizo kwa miaka mitatu kuanzia 2001-2004. Miongoni mwa makocha hao 24 tangu 2001 baadhi yao wamejirudia klabuni hapo.

Soma hapa orodha ya makocha watano ambao ndio waliodumu kwa muda mrefu ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi, wakiongozwa na Siang’a aliyekumbwa na mauti Septemba 9, 2016 akiwa na umri wa miaka 67.

JAMES SIANG’A-MIAKA MITATU

Kocha huyo Mkenya ndiye kinara wa kudumu kwa muda mrefu kuinoa Simba, kwani alidumua nao kwa miaka mitatu kuanzia 2001-2004 mfululizo akiandika rekodi ya kuifikisha timu hiyo kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 2003.

Simba ilitinga hatua hiyo ikiwa ni klabu ya pili baada ya Yanga kufanya hivyo mwaka 1998 tangu michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka kuwa Klabu Bingwa Afrika hadi Ligi ya Mabingwa kwa kuivua taji waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri.

Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Mtibwa Sugar, Moro United na Taifa Stars na enzi za uchezaji alikuwa kipa mahiri wa timu mbalimbali za Kenya ikiwamo Gor Mahia, aliondoka Simba akiweka heshima kwa kuipa timu hiyo ya Msimbazi ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu sambamba na taji la mwisho kwa klabu hiyo kwa michuano ya Kombe la Kagame 2002.

Kocha huyo aliachana na Simba mwaka 2004 kabla ya kukumbwa na umauti Septemba 9, 2016 kwao nchini Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu.

SOMA NA HII  CHAMA AWEKA REKODI YA KIBABE NYUMBANI

JOSEPH OMOG- SIKU 540

Kocha huyo kutoka Cameroon aliyeipa Azam FC taji pekee la Ligi Kuu Bara 2013-2014, ndiye anayeshika nafasi ya pili ya makocha walioinoa Simba kwa muda mrefu ndani ya miaka 21, akitumia jumla ya siku 540, ikiwa ni sawa na mwaka mmoja na nusu.

Omog, alijiunga na Simba Julai Mosi, 2016 kumpokea Jackson Mayanja kutoka Uganda aliyempokea kijiti Dylan Kerr kutoka Uingereza na alidumu na timu hiyo hadi Desemba 23, 2017 alipotemeshwa kazi kutokana na Simba kung’olewa kwenye michuano ya ASFC na timu ya Daraja la Pili (SDL, sasa First League) Green Warriors iliyokuwa Ligi Daraja la Pili kwa mikwaju ya penalti baada ya sare 1-1 kwa dakika 90.

Chini ya Omog, Simba ilibeba taji pekee la michuano ya Kombe la ASFC 2017 kisha kupewa mkono wa kwaheri aliposhindwa kuiongoza timu kwenye kulitetea kwa mara ya pili mfululizo.

PATRICK AUSSEMS- SIKU 499

Alifahamika kwa jina na Uchebe, kocha huyu kutoka Ubelgiji ndiye anayeshika nafasi ya tatu kwa kudumu muda mrefu ndani ya Simba ndani ya miaka 21 tangu 2001-2022.

Kocha huyu aliyekuwa kipenzi cha wachezaji na mashabiki, alidumu Msimbazi kwa siku 499 kwani aliajiriwa Julai 19, 2018 na kutimuliwa Novemba 2019.

Katika muda aliokaa Msimbazi, Aussems aliyepo AFC Leopards ya Kenya kwa sasa, aliipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2018-2019 na kuifikisha timu hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni rekodi tangu michuano ilipobadilishwa mwaka 1997.

Hadi mabosi wa Simba wanamtimua kocha huyo Novemba 30, 2019 ikiwa ni miezi mitatu tangu Simba ilipong’olewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na timu ya UD Songo ya Msumbiji aliiacha Simba ikiwa inaongoza msimamo wa ligi na kumrahisishia kazi kocha aliyempokea siku chache baadae.

SVEN VANDENBROECK- SIKU 392

Kocha huyu kutoka Ubelgiji na aliyempokea Patrick Aussems ndiye anayefuata katika orodha ya makocha waliodumu kwa muda mrefu Msimbazi, akitumia muda wa siku 392.

Sven aliajiriwa Desemba 12, 2019 ikiwa ni siku 12 tu tangu Aussems alipotimuliwa na alidumu na klabu hiyo hadi Januari 7, 2021 baada ya kupata dili nono katika Klabu ya FAR Rabat ya Morocco ikiwa siku chache tangu alipoiwezesha kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2020-2021 Akiwa ndani ya Simba, Kocha Sven aliyeiwezesha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC msimu wa 2019-2020 pamoja na kuipa Ngao ya Jamii na kuifikisha makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumtengenezea njia aliyempokea kikosini Mfaransa Didier Franco aliyeifikisha timu hiyo robo fainali ya michuano hiyo na kutetea pia ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, lakini ikapoteza Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.