Home Habari za michezo MGUNDA: UCHOVU ULIIMALIZA SIMBA SC…

MGUNDA: UCHOVU ULIIMALIZA SIMBA SC…

Kocha Msaidizi Simba SC

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema sababu ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC ni uchovu waliokuwa nao wachezaji wake baada ya kucheza mechi mfululizo bila kupata muda wa kutosha wa kupumzika.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza msimu huu na kocha huyo ameeleza kuwa kipigo hicho hapaswi kumlaumu mchezaji wala kiongozi yeyote sababu hayo ni matokeo ya mpira.

Mgunda alikiri mchezo ulikuwa mgumu na walijitahidi kupambana lakini wakajikuta wanapoteza pointi tatu ambazo waliingia uwanjani wakiwa na lengo la kuzichukua ili kurudi kileleni.

“Nawapongeze Azam kwa ushindi walicheza vizuri na walistaili kushinda, lakini kwa upande wetu tulijitahidi kwa kila namna tulitengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia ndio mchezo wa mpira unavyokuwa tumekubali matokeo na tunarudi kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo,” alisema Mgunda.

Kocha huyo alisema uchovu waliokuwa nao wachezaji wake pamoja na ratiba ngumu vinaweza kuwa sababu ya kushindwa kupata matokeo mazuri lakini hataki hicho kiwe kisingizio cha kupoteza mchezo huo.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Azam FC, Kally Ongala aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujitoa na kufanikiwa kupata ushindi huo ambao utawaongezea ari katika mechi zinazo kuja.

Kally alisema pamoja na ushindi lakini haukuwa mchezo rahisi kutokana na ubora waliokuwa nao Simba, ingawa anafurahi kuona vijana wake wamezitumia vyema mbinu alizowapa na kufanikiwa kupata matokeo hayo.

“Wakati napewa timu ari ya kupambana kwa wachezaji ilikuwa chini sana lakini baada ya uongozi kunikabidhi timu nilijaribu kuongea nao kwa utulivu na kuwataka kutumia fursa hiyo kuonesha uwezo wao nashukuru waliyafanyia kazi maelezo yangu,” alisema Kally.

Alisema ushindi huo hautowavimbisha kichwa bali wataendelea kupambana kupata matokeo mazuri sababu kwa ubora na maandalizi waliyofanya hawastaili kuwa kwenye nafasi waliyopo hivi sasa.

Kwa ushindi wa juzi Azam FC sasa imepanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14 sawa na Simba iliyopo nafasi ya tatu huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa kileleni mwa ligi hiyo kwa kukusanya pointi 20.

SOMA NA HII  KAZI IMEANZA YANGA.....GAMONDI ATAKA STRAIKA LA BILIONI 2.5...MABOSI YANGA WAKUNA KICHWA..