Home Habari za michezo NEEMA ZAZIDI KUMIMINIKA SIMBA…KAMPUNI NYINGINE YA MO DEWJI YAWEKA MZIGO MEZANI…

NEEMA ZAZIDI KUMIMINIKA SIMBA…KAMPUNI NYINGINE YA MO DEWJI YAWEKA MZIGO MEZANI…

KLABU ya Simba leo Oktoba 28,2022 imeingia mkataba wa miaka miwili wa bima ya afya na kampuni ya Mo Assurance ya Jijini Dar es Salaam.

Mkataba huo uliosainiwa una thamani ya Sh250 milioni kwa mwaka na utahusika kwa timu zote tatu za Simba kwa maana ya timu kubwa, timu ya Wanawake na Ile ya vijana.

Bima hiyo pia itawafikia waajiriwa wote wa Simba na familia zao ambapo kila mmoja atakuwa na nafasi ya kuongeza watu wanne tegemezi kwenye bima hiyo ambao ni mke/mume na watoto.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ameeleza namna timu hiyo itakavyonufaika na mkataba huo.

“Tumekuwa tukitumia gharama kubwa kwenye matibabu ya wachezaji na waajiriwa wengine wa Simba lakini ujio wa bima hii utatusaidia kwenye gharama hizo nakuongeza ufanisi kwa kila mtu kwenye eneo lake,” amesema Barbara.

Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya Mo Assurance, Fatema Dewji amesema mkataba huo umesainiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu huku akiamini utakuwa msaada kwa Simba na kampuni yake.

“Pande zote mbili tumejadili kwa muda mrefu kuhusu mkataba huu na Sasa tumesaini. Utasaidia katika matibabu na kuwafanya Wachezaji na waajiriwa wengine wa Simba kutowaza Tena suala la matibabu na kutimiza majukumu yao kwa kujiamini zaidi,” amesema Fatema.

Huduma ya Bima hiyo inapatikana kwenye hospitali zote kubwa nchini na itatumika kwa matibabu ya kawaida, kulazwa na majeraha yanayotokea mchezoni.

SOMA NA HII  YANGA WAMFANYIA KUFRU YA KIBABE MKUDE....KULIPWA MILIONI 150 KWA MWAKA..MKATABA WAKE HUU HAPA...