Home Habari za michezo BAADA YA YANGA KUSHINDWA KULIFURAHISHA TAIFA LEO…KAZI YATUA KWA SIMBA QUEENS…

BAADA YA YANGA KUSHINDWA KULIFURAHISHA TAIFA LEO…KAZI YATUA KWA SIMBA QUEENS…

Mechi ya kwanza ilikuwa ni ya kusoma mashindano lakini Simba Queens wametamba kwamba leo ndio wanaanza mashindano. Juzi walifungwa bao 1-0 na FAR Rabat ya Morocco huku wakikiwasha na Determine Girls ya Liberia.

Huo ni mchezo wa pili Kundi A kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyojizolea umaarufu mkubwa kwenye wiki za hivi karibuni kutokana na mashabiki kuvutiwa na kuwaona mastaa mbalimbali hususani wale wa Simba.

Simba Queens ambayo ndiyo wawakilishi wa Cecafa, watacheza mchezo huo leo saa 2 usiku Jijini Rabat na unatarajiwa kuwa mkali na ushindani mkubwa kwani timu zote zimeanza vibaya mechi zao za kwanza na kila mmoja ana usajili mzuri.

Determine wenyewe walifungwa mabao 4-0 na kuwa timu ambayo imeruhusu mabao mengi kundi A katika mechi za awali.

Upande wa uzoefu Determine ni kama Simba kutokana na wote hawana uzoefu wa michuano hiyo kwani ndio mara yao ya kwanza kushiriki ingawa zote ni mabingwa wa ligi zao za ndani.

Determine ilianzishwa mwaka 2007 na ilifuzu kwenda Morocco ikitokea upande wa Afrika Magharibi (WAFU) baada ya kutoka sare na AS Mande 1-1, 1-1 USPA na ikashinda 1-0 dhidi ya US Parcelles.

Simba inashika nafasi ya tatu katika kundi A ikiruhusu bao moja, nafasi ya kwanza inashikiliwa na Green Buffaloes ikiwa na pointi tatu huku ikifunga mabao manne na nafasi ya pili ni FAR Rabat ambao wana pointi tatu na bao moja.

Hata hivyo, wadau wa soka nchini walisema Simba Queens wanapaswa kuongeza umakini na kupambana zaidi.

Mtendaji Mkuu wa timu ya soka ya wanawake ya Ceasiaa Queens ya mkoani Iringa, Jumanne Mwanyiro alisema kinachotakiwa kwa wachezaji ni kucheza kwa kujituma mchezo unaofuata ili wapate matokeo mazuri.

“Wasikate tamaa waendelee kupambana lakini kubwa wacheze kwa kutafuta matokeo,”alisema Mwanyiro.

Mwenyekiti wa Baobab Queens, Innocensia Masawe alisema kinachotakiwa ni kufuata maelekezo ya kocha wa timu hiyo ikiwa ni pamoja na kutumia nafasi watakazozipata.

“Ugeni nao ni tatizo tumeshajifunza katika mchezo wa kwanza sasa ni lazima mchezo wa pili tuweke pembeni ugeni tupate matokeo,” alisema Masawe.

SOMA NA HII  WAKATI MASHABIKI WAKITAKA MAKUBWA CAF....MIPANGO YA FADLU NA SIMBA HII HAPA...