Home Habari za michezo DODOMA JIJI WARUDISHIWA FURAHA….KUWEKA HISTORIA NA YANGA…

DODOMA JIJI WARUDISHIWA FURAHA….KUWEKA HISTORIA NA YANGA…

Hatimaye burudani ya soka inarejea tena makao makuu ya nchi baada kupita mechi kadhaa za Ligi bila kuona timu yao ya Dodoma Jiji FC ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani, Jamhuri jijini Dodoma.

Uwanja wa Jamhuri ulifungiwa na Bodi ya Ligi kutokana na upungufu kadhaa ikiwemo sehemu ya kuchezea, hivyo kukosa sifa za kuandaa mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu na kuifanya Dodoma Jiji kuhamia Uwanja wa CCM Liti mjini Singida.

Katika mechi nne za ligi ambazo Dodoma Jiji imecheza Uwanja wa CCM Liti imeambulia alama tatu pekee na kupoteza mechi tatu.

Timu hiyo ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City FC, wakachapwa 2-1 na Tanzania Prisons FC, wakafungwa 1-0 na Mtibwa Sugar huku wakishinda 1-0 dhidi ya Geita Gold FC na kuruhusu alama tisa kuondoka nyumbani.

Habari njema sasa ni Uwanja wa Jamhuri kukamilika na timu hiyo itaanza kuutumia Novemba 22 dhidi ya Yanga. Pia itaweka historia kwa mara ya kwanza Yanga kucheza usiku mikoani.

Akizungumza jijini Arusha, Katibu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema changamoto kubwa iliyokuwepo ni uchakavu wa sehemu ya kuchezea na tayari wameifanyia kazi, na kwamba hivi sasa kila kitu kiko sawa.

“Tumefanya kazi kubwa kutengeneza sehemu ya kuchezea na changamoto tuliyoipitia pia ni maji ambayo yalikuwa yanaingia katika uwanja yalikuwa ni kiasi kidogo.

“Tulikaa chini na wamiliki wa uwanja kama sisi Dodoma Jiji tukachimba visima na changamoto hiyo haipo kwa sasa. Pia tumeziba mitaro iliyokuwa inapitisha maji pembeni ya uwanja na sasa tuko tayari,” alisema Fortunatus.

Aliongeza kuwa Ligi Kuu Bara msimu huu ni ngumu kwa sababu kila timu imejiandaa vilivyo, lakini kama uongozi bado wanapambana kuhakikisha wanarejesha makali na kutimiza azma ya timu kumaliza katika nafasi tano za juu.

SOMA NA HII  MBINU HII INAYOTUMIWA NA TFF DHIDI YA SIMBA NA YANGA...YATUMIWA KWA PSG YA UFARANSA..