Home Habari za michezo HIZI HAPA SIKU 60 ZA NDOA YA MGUNDA NA SIMBA…KAWEKA NA KUVUNJA...

HIZI HAPA SIKU 60 ZA NDOA YA MGUNDA NA SIMBA…KAWEKA NA KUVUNJA REKODI KIBAO ZA WAZUNGU…

Kocha Msaidizi Simba SC

Kama hujui ni kwamba jana ilitimia miezi miwili kamili ambayo ni sawa na siku 60, tangu kocha Juma Mgunda atue Msimbazi kuinoa Simba na kuweka heshima ya kibabe.

Simba ilimtambulisha kocha huyo iliyemchukua kutoka Coastal Union ili kukaimu nafasi ya kocha mkuu kuziba nafasi iliyoachwa na Mserbia Zoran Maki aliyesitisha ghafla mkataba na kuibukia Al Ittihad ya Misri.

Kutua kwa kocha huyo Msimbazi zilikuwa taarifa zilizoshtua na kuwagawa mashabiki wa Simba, baadhi wakiamini Mgunda hakuwa anatosha kuinoa timu hiyo na hasa baada ya kutaniwa na watani wao, kwamba klabu yao imeishiwa na haina uwezo wa kupata kocha mzuri ndio maana ikaamua kwenda kuwaazima Wagosi wa Kaya kocha wao.

Mgunda mwenyewe aliyasikia hayo na mengine mengi na kuamua kuwajibu kwa vitendo kwa kuifanya Simba kucheza kwa ubora, jambo lililowafanya miongoni mwa mashabiki wa chama hilo na wadau wengine wa soka kumpigia chapuo apewe timu jumla kama kocha mkuu.

Makala hii inaakuletea Mgunda alivyotimiza siku 60 ndani ya Simba na namna alivyowafunga midomo waliokuwa wakimchukulia poa, kwani rekodi zake ni tamu na zinaonyesha kumbe makocha wazawa wakiaminiwa wanaweza kufanya makubwa kuliko hata makocha wa kigeni.

ALIANZIA HAPA

Mara tu baada ya kutua Simba siku iliyofuata Mgunda aliungana na kikosi cha Msimbazi kwenda nchini Malawi kucheza mechi ya mtoano ya mkondo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya nchini humo.

Siku mbili mbele akaiongoza Simba kutupa karata ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu na kushinda 2-0 ugenini mabao yakifungwa na Moses Phiri na nahodha John Bocco kisha kurejea nchini.

Baada ya kurudi Bongo alisafiri na Simba kwenda Mbeya kucheza mechi ya ligi dhidi ya Tanzania Prisons na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Jonas Mkude dakika ya 90 na kuvunja mwiko wa Simba kutopata ushindi mbele ya Prisons ugenini tangu 2019.

Mchezo huo ulivyomalizika kikosi kilirudi Dar es Salaam kujipanga na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets.

Mechi hiyo ilipigwa Septemba 18 Uwanja wa Mkapa, Simba ikishinda mabao 2-0 kwa mabao ya Phiri aliyefunga yote na kutinga hatua ya pili ya mtoano kwa jumla ya mabao 4-0.

Wakati akiwa na furaha ya kushinda mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao akifunga jumla ya mabao matano, aliipeleka Simba Zanzibar kucheza mechi mbili za kirafiki ili kukijenga zaidi kikosi chake na kushinda zote.

Mechi ya kwanza Zenji aliiongoza Simba Septemba 25 kuivaa Malindi na kushinda bao 1-0 lililofungwa kwa kichwa na Nassoro Kapama akiunganisha mpira wa kona na mechi ya pili kuichapa Kipanga mabao 3-0 yakifungwa na Augustine Okrah aliyefunga mara mbili na moja likitupiwa nyavuni na Kibu Denis.

Baada ya mechi hizo mbili, Simba ilirejea Dar es Salaam na Oktoba 2 ilicheza mechi ya ligi na Dodoma Jiji na kushinda 3-0 kwa mabao ya Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyejifunga, Phiri na Habib Kyombo.

Kilichofuata hapo kikosi kilijifua kwa siku tatu kisha kusafiri kwenda nchini Angola kucheza mechi ya kwanza ya duru ya pili ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Premiero De Agosto ya nchini humo na kushinda 3-1 mchezo uliopigwa Oktoba 9, mabao ya Simba yakifungwa na Clatous Chama, Israel Mwenda na Phiri.

Timu ilirejea nchini baada ya hapo na kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi ya marudiano iliyopigwa kwa Mkapa Oktoba 16 na Simba ya Mgunda kushinda 1-0 bao la Phiri na kutinga moja kwa moja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa 4-1.

Pamoja ya kutinga makundi, hapohapo Mgunda alianza kupiga hesabu za mchezo wa ligi dhidi ya watani wa jadi Yanga, mechi iliyochezwa Oktoba 23 kwa Mkapa, Simba ikiwa ugenini na kutoka sare ya bao 1-1 bao la Mnyama likifungwa na Okrah kabla ya wana Jangwani kusawazisha kupitia kwa Aziz Ki.

Siku tano baada ya pambano hilo la watani wa jadi Mgunda alikutana na kipigo chake cha kwanza ndani ya Simba kwenye mechi iliyopigwa Oktoba 27 Uwanja wa Mkapa. Simba ikiwa ugenini ilipoteza kwa kufungwa 1-0 na Azam kwa bao la Prince Dube.

Ni kama matokeo hayo yalimpa hasira Mgunda na vijana wake na kwenda kuzimalizia Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ligi iliyopigwa Uwanja wa Mkapa na kushinda mabao 5-0 yakifungwa na Mzamiru Yassin, Pape Sakho aliyefunga mawili, Phiri na Okrah. Huo ni ushindi wa kwanza mnono kwa Simba msimu huu katika Ligi Kuu Bara na pia ushindi mkubwa kutokea kwenye ligi ya msimu huu.

REKODI CAF

Tangu mwaka 1998, Hayati Tito Mwaluvanda alipoifikisha Yanga hatua ya makundi kwenye ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa ni Mgunda aliyefika hatua hiyo kwa upande wa makocha wazawa.

Zari la Mgunda linafanana na la Mwaluvanda ambaye alifika hatua hiyo akiwa kocha wa muda au unaweza kusema kaimu na msaidizi wake alikuwa Fred Felix ‘Minziro’, baada ya Yanga kumtimua aliyekuwa kocha mkuu, Mwingereza Steve McLennan.

Hata hivyo, upande wa Kombe la Shirikisho Afrika mzawa pekee aliyeipeleka timu hatua ya makundi ni kocha Seleman Hemed ‘Moroco’ akiwa na Namungo FC.

AWAFUNIKA WAGENI

Mgunda pia amewafunika makocha wageni kwa kuifunga Prisons timu ambayo imekuwa ngumu kwa Mnyama akishindwa kupata ushindi katika miaka mitatu ya hivi karibuni ugenini chini ya makocha tofauti.

Kabla Simba ya Mgunda kushinda bao 1-0 ugenini mbele ya Prisons, mara ya mwisho Simba kupata ushindi ugenini dhidi ya wajelajela hao ilikuwa msimu wa 2018/2019 chini ya kocha Mbelgiji Patrick Ausems ikishinda 1-0 na baada ya hapo haikushinda iliambulia suluhu moja tu msimu uliofuata (2019/20) chini ya Kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck lakini haikuepuka kichapo kwani msimu uliofuta 2020/21 ilikubali kichapo cha bao 1-0 na msimu uliopita Simba ikiwa chini ya Seleman Matola kwa muda ikachapwa 1-0.

MSIKIE MWENYEWE

Akizungumzia siku hizo, Mgunda anaeleza kufurahia uwepo wake ndani ya Simba na kufichua siri ya mafanikio yake hayo kuwa ni ushirikiano mzuri anaoupata kutoka kwa viongozi, wasaidizi wake, wachezaji na mashabiki.

“Nafurahi kuwa hapa na kubwa zaidi nafurahi timu inapofanya vizuri,” anasema kocha huyo.

“Nawashukuru wachezaji wote kwa ushirikiano wao na kujitoa kupambania timu ili ifikie malengo sambamba na viongozi wa juu, wenzangu wa benchi la ufundi na mashabiki na naamini kwa mwendo huu tutafikia malengo kwa pamoja,” anasema Mgunda.

Mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni anamuelezea Mgunda kuwa kocha mzuri na atafanya vyema zaidi kama atapewa ushirikiano kutoka kwa kila mtu.

“Ni kocha mzuri na amethibitisha hilo akiwa Simba. Kinachotakiwa ni wakuu wake kumpa ushirikiano wa kutosha na sapoti kubwa ili aifikishe timu kwenye malengo yake,” anasema.

Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anamuelezea Mgunda kuwa kocha mzuri anayependa mafanikio.

“Ni kocha mzuri na tunamsikiliza na kutenda kile anachotueleza. Ni mchangamfu na anajua anachokifanya na ana malengo makubwa,” anasema Tshabalala.

Mchezo unaofuata wa Simba itacheza Jumatano ijayo na Singida Big Stars ugenini kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.

SOMA NA HII  BARBARA ATOBOA SIRI...USAJILI WA ADEBAYO KUTUA SIMBA