Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA WATUNISIA…RAGE AIBUKA NA HAYA KWA YANGA…ATOA MKANDA MZIMA WA...

KUELEKEA MECHI NA WATUNISIA…RAGE AIBUKA NA HAYA KWA YANGA…ATOA MKANDA MZIMA WA FIGISU ZAO…

Habari za Simba

Kigogo mmoja wa Simba, amekiangalia kikosi cha Yanga kilichocheza na Club Africain na kutoka suluhu, kisha akaichorea ramani kwa mchezo wa marudiano akiamini kama watazitumia vyema basi watakuwa na nafasi kubwa ya kuwangoa Watunisia licha ya kwenda kucheza ugenini.

Kikosi cha Yanga kinachotarajiwa kuondoka nchini leo Ijumaa kuwahi pambano hilo litakalopigwa Jumatano kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Olympique Hamadi Agrebi, mjini Tunis, kililazimishwa suluhu na Watunisia hao katika mechi ya kwanza ya mtoano wa Kombe la Shirikisho.

Suluhu hiyo imeonekana kama kuwavuruga Wanayanga ambao wameanza kuushambulia uongozi na kuwashutumu wachezaji, lakini Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amewapa mbinu Yanga ili kuweza kuwatoa wenyweji ugenini akisema kila kitu kinawezekana.

Rage aliwachorea ramani Yanga, huku akiwataka mashabiki, viongozi na mastaa wa Yanga kutokata tamaa na matokeo ya juzi nyumbani kwa kuwaambia mchezo huo ulikuwa ni mgumu kwa Yanga kutokana na wapinzani wao kujilinda muda mwingi na kutowapa uhuru wa kupenya.

“Ukiangalia jinsi ambavyo Africain, ilivyocheza utaona ilikuwa na wachezaji tisa wakijilinda, hivyo lazima mashabiki walione hilo bila kuanza kulaumu wachezaji,” alisema Rage na kuongeza, Yanga haikucheza vibaya kama wengi wanavyodhani isipokuwa wapinzani wao walikuja na mkakati mzuri wa kujilinda na kufanikiwa japo mchezo kiujumla haujaisha.

“Yanga inanufaika na 0-0 kwani ugenini ikitoka sare ya mabao inawavusha kwa hatua inayofuata, hivyo wajiandae vizuri kwani nafasi ipo na timu nyingi zimeshashinda ugenini, kwani najua Africain itafunguka kusaka mabao na watani zangu watumie nafasi hiyo kuimaliza mapema,” alisema Rage.

Rage alisema licha ya rekodi kuwabeba Waarabu wanapokuwa nyumbani kwao, lakini Yanga ikiondoka na mikakati tofauti na ilivyiocheza Dar itashinda kwani soka la kisasa limebadilika na haijalishi unacheza nyumbani au ugenini.

KIPANGA HAWA HAPA

Wakati Rage akiyasema hapo, Kipanga iliyotolewa na Africain kwenye raundi ya kwanza, imeitaka Yanga kujiandaa kubabiliana na fitina za nje ya uwanja kwa wapinzani wao, lakini ikikomaa itatoboa freshi tu.

Nyota wa Kipanga waliopigwa 7-0 katika mechi ya marudiano mjini Tunis baada ya suluhu ya nyumbani, walisema Yanga ikitulia ina uwezo wa kuwashangaza Watunisia waliowataja kama timu yenye fujo na fitina za soka ikikicheza nyumbani.

“Kama Yanga itajipanga itaifunga, iache kufikiria fitina na fujo zao, wao wapambane uwanjani kutafuta matokeo tu,” alisema nyota wa Kipanga, Abdillah Suleiman Kombo ‘Mido Kubwa’.

Kombo alisema ukiachana na matokeo ya karibuni ya kimataifa, timu hiyo sio tishio sana kwenye ligi yao huku akifichua Yanga inachotakiwa ni kuidhibiti dakika 30 za kipindi cha kwanza na ikiweza kufunga tu itawamaliza, japo itapata upinzani kutoka kwa mashabiki.

“Wakiwa wanaongoza, hata waokota mipira wanajichelewesha kuwapa mipira, pia mashabiki wao wana fujo hadi za kurusha chupa uwanjani, lakini Yanga wala wasizingatie, ingawa kwenye usalama askari wao wako vizuri.

“Vyumba vya kubadilishia nguo pia hakuna shida na hata hotelini, kuna ulinzi, sisi tulipokwenda askari wao walikuwa wengi na walitulinda kuhakikisha hatupati tatizo kuanzia hotelini hadi tunaingia uwanjani,” alisema Kombo huku kocha wa timu hiyo, Hassan Kitimbe alisema kama Yanga itawamudu na kuwabana kipindi cha kwanza na kuwafunga bao la mapema, nafasi ya kusonga ipo kwa wawakilishi hao wa Tanzania.

MSIKIE NABI

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, amekiri presha kwake kwa sasa ni kubwa baada ya matokeo ya juzi Jumatano, lakini ametangaza kujivisha mabomu kwa mchezo wa ugenini akisema watamalizana nao huko huko.

Nabi alisema mbinu za Watunisia kucheza kwao wengi nyuma ya mpira kuliwapa wakati mgumu kufungua ukuta wao na kwamba bado matokeo hayo sio mabaya watakwenda kupambana ugenini hukohuko akisema watashambulia mwanzo mwisho.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuwaona wanacheza hivi, waulizeni hata ile timu ya Zanzibar watawaambia hili, hii ni klabu ambayo naijua tulishindwa kuufungua ukuta wao kama ambavyo tulijipanga, hata tulipojaribu njia nyingine bado walikuwa wengi,” alisema Nabi mwenye asili ya Tunisia.

“Hii mechi haijaisha nimeshangaa kuwaona watu wanaona kama tumefungwa, nakubaliana na suala moja tu tumeshindwa kushinda nyumbani lakini sare hii inatupa faida zaidi Yanga kuliko wapinzani wetu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Mimi ni kocha ambaye sina mbinu za kujilinda na kucheza kwa kujihami, hatutapaki basi kwa kucheza wengi nyuma. Tutakwenda kushambulia na kuwa makini kujilinda, kwani hatuna cha kupoteza nawaamini wachezaji wangu tutapata mabao ugenini.”

SOMA NA HII  WAKATI OKWA AKITUA NA MZUKA WA KINIGERIA SIMBA...MANZOKI AIBUKA NA KUKOLEZA UKAKASI WA DILI LAKE...