Home Habari za michezo “NITAKA JEZI YA MANULA…PALE SIMBA NAMBA YANGU IKO ….”

“NITAKA JEZI YA MANULA…PALE SIMBA NAMBA YANGU IKO ….”

“Natamani nicheze na Aishi Manula.” Ni kauli ya kipa namba moja wa Tanzania Prisons, Hussein Abel akielezea ndoto zake za kucheza soka katika timu kubwa na wachezaji wa viwango vya juu, huku akisema pale Simba anapata namba.

Abel ambaye ni mchezaji pekee wa Ligi Kuu kwenye kijiji cha Songabatini wilayani Muheza mkoani Tanga, amekuwa mmoja wa makipa bora nchini akiacha historia katika kazi yake hiyo uwanjani.

Kipa huyo aliyeanza soka la ushindani tangu 2014 akiichezea Madini FC ya jijini Arusha ilipokuwa daraja la pili (kwa sasa First League) amekuwa msaada mkubwa tangu alipotua Tanzania Prisons msimu uliopita.

Katika mahojiano maalumu , Abel amefunguka mengi ikiwamo tamu na chungu alizokutana nazo katika kazi ya soka ndani na nje ya uwanja na matamanio yake kuzichezea Simba, Yanga na Azam.

MSIMU MGUMU

Kipa huyo aliyejiunga na Wajelajela hao katika dirisha dogo msimu uliopita akitokea Taifa Jang’ombe ya Zanzibar, anasema hatasahau ligi ya msimu uliopita kutokana na magumu aliyokutana nayo. Alicheza mechi 13 zikiwamo za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kwamba haikuwa kazi rahisi kuinusuru timu hiyo ili kubaki Ligi Kuu.

“Niliona kabisa rekodi yangu inarudi ya kushusha timu kwa sababu nakumbuka msimu 2018/19 nilipoipandisha Sahale All Stars daraja la kwanza tulishuka tena. Hivyo nikawaza sana, lakini nikajipa matumaini,” anasema Abel.

Akizungumzia mchezo wao wa mchezo mchujo (play off) dhidi ya Mtibwa Sugar msimu uliopita ambao pia walinusurika na kubaki Ligi Ku, anasema: “Kwanza yale mabao sikuyaelewa walivyotufunga (Mtibwa 3-1) ikiwamo bao la Salum Kanoni yalikuwa kama ya miujiza. Kwa hiyo nikaona dalili za Prisons kushuka daraja licha ya kushinda mechi ya marudio bao 1-0 tukaangukia kwa JKT Tanzania ya Championship.

“Ile mechi na JKT Tanzania tuliposhinda ugenini akili ikatulia, japokuwa ile ya marudiano hapa Sokoine walikuwa wakali na mwenzangu Edward Mwakyusa alifanya kazi nzuri na kuibakiza timu Ligi Kuu, ila msimu ulikuwa mgumu sana.”

YANGA YAMPA ULAJI

Abel anasema baada ya kukosa namba Coastal Union alishauriwa na mchezaji mwenzake Adil Sultan kwenda kusaka maisha Zanzibar na kufanikiwa kupata Taifa Jang’ombe.

“Ndio ikafika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na nikabahatika kucheza mechi hiyo (dhidi ya Yanga), ila kocha hakutaka alishinikizwa na mashabiki,” anasema Abel.

“Kocha alihitaji amchezeshe kipa mwenzangu Aboubakari Abas, lakini nashukuru nilifanya vizuri japokuwa tulipoteza hiyo mechi, ila kazi ilikuwa nzuri kwa sababu baada ya mchezo nilipata ofa nyingi timu za Ligi Kuu.”

MANULA AMKOSHA

Mchezaji huyo anasema makipa wengi Ligi Kuu wanafanya vizuri na kwa viwango bora, lakini kwake Manula ni namba moja. “Kwa ujumla Manula namkubali sana. Siyo kwamba wengine hawafanyi vizuri la, ila huyu ni namba moja anajua sana. Hata hivyo natamani siku moja nicheze naye timu moja haijalishi Simba au kwingine,” anasema Abel.

Mkali huyo anaeleza kuwa moja ya ndoto zake mbeleni ni kucheza moja ya timu kubwa kati ya Simba, Yanga au Azam na popote watakapomuita anaamini anaweza kupata namba kikosini. “Kwa sasa kati ya timu hizo naona Simba naweza kupata namba. Ni ndoto yangu kucheza moja ya klabu hizo pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars,” anasema Abel.

PRISONS MSIMU HUU

Abel anasema baada ya msimu uliopita kucheza kwa presha kwa sasa anaiona timu ni bora kutokana na mabadiliko liliyofanya benchi la ufundi.

Anafafanua kuwa licha ya mkataba wake kuwa ukingoni, lakini iwapo watahitaji kuendelea naye hana tatizo, huku akifurahia maisha ndani na nje ya timu.

“Msimu huu tuko imara na bora sana ukilinganisha uliopita ambapo tulipitia mazito ikiwamo mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha kwani kila mmoja alikuja na falsafa yake,” anasema Abel.

“Mkataba wangu unaisha ikifika dirisha dogo. Kwa muda niliokaa Prisons kwa ujumla ni timu isiyo na janja janja. Mazingira ni mazuri kuanzia kambini hadi kwenye maslahi, wakitaka niendelee sina tatizo.”

AKUMBUKA MLEZI WAKE

Mchezaji huyo anasema mojawapo wa watu ambao hawezi kuwasahau ni mlezi wake Twaha Hassan ambaye aliamua kumsaidia muda wote bila kujali hawafahamiani.

“Yule mzee hakunifahamu, ila alipenda kazi yangu akanipeleka kwake nikaishi na kunipa nauli za kuhudhuria mazoezi, lakini hata Kocha Kesy Abdalah aliyenikuza na kunipa mwelekeo pamoja na yule mchezaji, Sultan aliyenilipia nauli kwenda Zanzibar,” anasema.

Abel anasema katika familia yao walizaliwa wanne na yeye alibahatika kucheza soka, lakini mama mzazi hakutaka ajiingize kwenye ishu ya mpira, bali kusoma.

Anasema baba alikuwa askari hivyo mambo ya mpira hakuyapa kipaumbele kabla ya kifo chake.

“Baadaye wazee pale vijijini wakaanza kumshauri (mama) aniache niendeleze kipaji changu na hadi sasa ni mmoja wa watu wanaoniombea sana kwenye kazi yangu,” anasema Abel ambaye haamini katika imani za kishirikina kwamba wachezaji wanapigana misumari.

“Hizo za misumari sijui kabisa japokuwa huwa nasikia. Binafsi haijawahi kunikuta, ikitokea nimeumia najua kabisa ni kawaida na huwa natibiwa narudi ndani ya muda mfupi.”

NJE YA SOKA

Abel bado hajaoa, lakini ana mtoto wa kike na mipango yake ndani ya mwaka huu anaweza kufunga pingu za maisha na ampendaye.

Kuhusu vyakula, yeye ni mpenzi wa ugali, mbogamboga na matunda, huku akieleza kuwa kiatu anachovaa ni chapa ya Nike namba 10 na kama mkwanja utasoma vizuri mbeleni anatamani amiliki gari kali.

“Napokuwa likizo sipendi kukaa sehemu ya kelele nyingi. Napenda utulivu, nimepanga Mungu akijaalia nitafunga ndoa ndani ya mwaka huu kwa sababu mchumba ninaye tayari,” anasema.

KIKOSI CHAKE BORA

Anataja kikosi chake kuwa Aisha Munula, Isra Mwenda, Ibrahim Abraham, Dickson Job, Enock Hinonga, Jonas Mkude, Hamis Kanduru, Clatous Chama, Jeremiah Juma, Omary Omary na Benard Morison ambao watakuwa chini ya Kocha Hanour Janza.

SOMA NA HII  RAIS WA FIFA NA CAF KUZISHUHUDIA SIMBA NA YANGA KESHO KUTWA....MAJALIWA AWAOA NENO LA KUZINGATIA...