Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA KESHO…NABI ATOA KISINGIZIO MAPEMA….AWATUPIA LAWAMA TFF KWA ‘KUMSINCHI’…

KUELEKEA MECHI YA KESHO…NABI ATOA KISINGIZIO MAPEMA….AWATUPIA LAWAMA TFF KWA ‘KUMSINCHI’…

Habari za Yanga

Wakati kikosi cha Yanga kikishuka uwanjani kesho kwenye mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania nafasi ya kutinga makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain ya Tunisia, Kocha Mkuu wa timu hiyo Nasreddine Nabi amelalamikia ugumu wa ratiba unaowakabili.

Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam, Nabi amesema kutokana na ugumu wa ratiba inayowakabili waliomba kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuondolewa baadhi ya michezo yao ila bahati mbaya kwao hawakuweza kujibiwa chochote.

“Mchezo wetu na Geita Gold tuliomba uondolewe ili tupate muda mzuri wa kujiandaa kama ambavyo mashirikisho mengine yanafanya kwa timu zao ila hatuwezi kulalamika sana juu ya hilo kwani akili zetu tunazielekeza kesho kupata matokeo chanya.” alisema Nabi.

Nabi aliongeza licha ya changamoto hizo zote amekiandaa kikosi chake vizuri kwenye mchezo huo kwani malengo yao ni kufuzu hatua inayofuata.

“Kuna wachezaji wawili watakaokosekana kesho kutokana na majeraha waliyoyapata dhidi ya Geita Gold ila siwezi kuwataja hapa kwa sababu za kiufundi ila wengine wote waliobaki wako fiti kuipambania timu yao.”

Yanga imefika hatua hii baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili tu ya mtoano na Al Hilal Omdurman kutoka Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Kwa upande wa Club Africain hii ni mara ya pili mfululizo inarudi Tanzania kwenye mashindano haya baada ya Oktoba 8, mwaka huu kucheza na Kipanga ya Visiwani Zanzibar katika Uwanja wa Amaan na kutoka suluhu.

Hata hivyo suluhu hiyo kwa wawakilishi hao wa Tanzania haikuwasaidia kutinga hatua inayofuata baada kukubali kichapo cha cha mabao 7-0 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa nchini Tunisia Oktoba 16.

Yanga inahitaji ushindi mzuri nyumbani ili kujiweka kwenye mazingira salama kabla ya kurudiana tena Novemba 9, katika Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic nchini Tunisia.

Yanga ambao ndio wawakilishi pekee kwenye michuano hii ya Shirikisho Afrika kufuatia Azam na Geita Gold kutolewa wanaisaka rekodi yao ya kuingia makundi kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 2016 na 2018.

Mshindi wa jumla baina ya timu hizi atakata tiketi ya kufuzu moja kwa moja kwenye hatua ya makundi Shirikisho Afrika ambapo mechi zake zitaanza kupigwa rasmi kuanzia Februari Mwakani.

SOMA NA HII  BREAKING NEWS : KOCHA WA YANGA AFARIKI DUNIA