Home Habari za michezo MAHITAJI YA MOSES PHIRI SIMBA YASHTUA….ATAKA MAMBO KAMA YA OKWI NA KAGERE…

MAHITAJI YA MOSES PHIRI SIMBA YASHTUA….ATAKA MAMBO KAMA YA OKWI NA KAGERE…

Habari za Simba

Kinara wa mabao Simba, Moses Phiri amewatahadharisha wachezaji wenzake akiwaambia kazi haijaisha licha ya timu hiyo kufanya vyema nyumbani na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Phiri mwenye mabao 10 aliyoifungia timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara na ile ya Afrika, alisema licha ya kutupia vya kutosha lakini havimbi kichwa na wala hataki wenzake kudhani kazi imeisha kwa vile bado wana kibarua kigumu kwenye hatua ya makundi ya CAF.

Mzambia huyo amefunga mabao matano ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, KMC, Geita Gold, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji na mengine kama hayo katika Ligi ya Mabingwa, yakiwamo matatu dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi na mawili ilipoing’oa Primeiro de Agosto ya Angola na kuivusha Simba.

Phiri alisema kasi hiyo inampa nguvu ya kuendelea kuzisakama nyavu kama alivyosisitiza ndio kwanza kazi inaanza, kitu kikubwa anachokizingatia ni umakini na kuongeza bidii na kuwataka mastaa wenzake wasilale kwa kuamini kazi imeisha.

“Kuna ushindani kwenye ligi ya ndani na michuano ya CAF, unahitajika umakini wa hali ya juu, kuhakikisha tunafanya mambo makubwa kwenye majukumu yote yaliopo mbele yetu, kwa sababu kadri tunavyojipanga ndivyo wapinzani wetu wanavyojipanga vilevile,” alisema Phiri aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Zanaco ya Zambia.

“Jambo kubwa ninalotamani msimu wangu wa kwanza kucheza Simba ni kupata mafanikio makubwa ambayo yatakuwa alama ya kuonyesha mchango wetu kwa klabu naamini hiyo ni ndoto ya kila mchezaji kuona anamaliza kwa kicheko,” aliongeza mkali huyo ambaye alipewa ushauri wa bure na staa wa zamani wa timu hiyo, Ulimboka Mwakingwe aliyesema kwa mwanzo aliyoanza nao anaweza akajitengenezea ufalme wake kama ilivyokuwa kwa mastaa wengine waliopita kama Meddie Kagere anayekipiga Singida Big Stars.

Alisema mashabiki wa Simba walikuwa wanamuimba Emmanuel Okwi, lakini Kagere alipindua meza kwa kuchukua kiatu cha dhahabu mara mbili mfululizo, hivyo akiwa anazungumzwa kila kona, jambo analoliona anaweza akalifanya Phiri.

“Kila mchezaji ana mchango wake, wengi walikuja Simba na kuondoka ambao walifanya vitu vinavyosimuliwa kuanzia miaka hiyo na sasa, hilo liwe chachu kwa wachezaji kujituma ili na wao wawe na cha kusimuliwa,” alisema Mwakingwe anayeinoa Pamba.

SOMA NA HII  ACHANA NA YANGA KUUPIGA MWINGI DHIDI YA WATUNISIA..ILA KAMA SIO LOMALISA NA FARIDI WANGEUMBUKA..