Home Habari za michezo NABI APANIA KUITIKISA AFRIKA…ATAJA MASHINE MPYA ZA KUONGEZA NGUVU YANGA…

NABI APANIA KUITIKISA AFRIKA…ATAJA MASHINE MPYA ZA KUONGEZA NGUVU YANGA…

Habari za Yanga SC

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Disemba 15, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema ataleta mashine tatu kwa ajili ya kuboresha kikosi chake.

Nabi alisema malengo yake ni kushinda taji la Ligi Kuu mfululizo na kufanya vyema kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nabi alisema kabla ya mchezo wa Dodoma Jiji leo Jumanne, alifanya kikao kifupi na wachezaji wake kuwaeleza kila mmoja anatakiwa kupambana kwenye nafasi yake kwani hatapenda kuona wengine akiachana nao baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Disemba 15.

Kocha huyo raia wa Tunisia alisema jambo la kwanza atakalolifanya kuna wachezaji ambao hawakuwa wanacheza mara kwa mara nao atawapa nafasi ili kuonyesha wanastahili kuendelea kubaki ndani ya timu.

“Baada ya hapo nitafanya tathimini ya mwisho na kupata wachezaji wa kubaki, kuachana nao na wale wapya ambao wataingia kwenye timu na watakuwa wanacheza kwenye maeneo tofauti,” alisema Nabi na kuongeza;

“Lazima tuongeze nguvu kwenye dirisha dogo la usajili kwani tunakwenda kwenye Mashindano ya CAF, yenye timu bora na wachezaji wenye ubora tunahitaji kufanya vizuri ndio maana tunaboresha kikosi chetu,”

“Bado sijafanya maamuzi ya maeneo gani nitaongeza wachezaji wapya hadi hapo nitakapowapa nafasi wote waliopo kwenye timu kucheza ila tunakwenda kwenye soko la usajili kutafuta wachezaji wenye viwango bora.

Nabi alisema kikosi chake kila nafasi moja kuna wachezaji wawili hawapishani mno kwenye viwango vyao kwahiyo akikosekana mmoja mwingine anakwenda kufanya kazi vizuri jambo kama hilo timu nyingi za ligi hazina.

Alisema kuna baadhi ya mechi amekuwa akiwapumzisha wachezaji wake wa kikosi cha kwanza na aliwapa nafasi wengine waliokwenda kufanya vizuri na kupata matokeo bora kama ilivyokuwa mechi ya Kagera Sugar.

“Kufanya mabadiliko na kuendelea kupata matokeo mazuri si jambo dogo nawapongeza wachezaji wote ukiachana na kikosi cha Yanga sioni timu nyingine inayoweza kufanya hivyo na ikaendelea kupata matokeo mazuri,” alisema Nabi na kuongeza;

“Ili tuweze kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu tunapaswa kupata matokeo mazuri dhidi ya timu zenye malengo ya kutwaa ubingwa kama Simba, Azam na Singida Big Stars na bahati nzuri kwetu hakuna hata mchezo mmoja tuliopoteza dhidi ya vigogo hao msimu huu,”

“Kwenye kipindi cha hivi karibuni nimekuwa nikifurahishwa na kiwango cha Joyce Lomalisa amekuwa akifanya kazi nzuri ya kulinda na kushambulia kama majukumu ya nafasi yake ilivyo.

“Awali alikutana na maneno mengi kutokana na kushindwa kuzoea mazingira mapya kwa haraka ila baada ya kuzoea ligi, wachezaji wenzake, viwanja na mazingira yote ndani na nje ya timu anafanya vizuri amekuwa mchezaji muhimu.”

SOMA NA HII  WAARABU WAINGIA MAZIMA MAZIMA KWA ONANA....KUTUMA OFA NONO KWA SIMBA KUMBEBA..