Home Habari za michezo SAA MOJA KABLA YA KUKIPIGA NA WAARABU…MATOKEO YAIBEBA YANGA..NABI AINGIA KININJA…

SAA MOJA KABLA YA KUKIPIGA NA WAARABU…MATOKEO YAIBEBA YANGA..NABI AINGIA KININJA…

Habari za Yanga SC

YANGA ina dakika 90 pekee za kutunza heshima yake kimataifa Jijini Tunis leo saa 1 usiku kwa kupata matokeo ya kufuzu makundi ya Shirikisho watakapocheza na Club Africain katika mechi ya marudiano. Ili Yanga ifuzu inahitaji sare yoyote ya mabao au ishinde mchezo huo baada ya kutoka suluhu Dar es Salaam. Ili kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya hali ya hewa, Yanga iliwahi Tunisia kuweka kambi maalumu kwenye mji wa Sousse kabla ya juzi jioni kwenda Tunis.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alieleza kuwa kikosi kipo kwenye morali na wapo tayari kupindua meza ugenini na kutinga makundi.

Japo Yanga haina rekodi za kutisha michuano ya CAF, lakini imeweka heshima ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti kuwa timu pekee ya Tanzania kufika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika – tena mara mbili.

Yanga imewahi kutinga hatua hiyo ikianza msimu wa 2016 ikiingia kwa kuchomolewa Ligi ya Mabingwa na kupenya katika mchujo wakiifunga Sagrada Esperanca ya Angola nyumbani mabao 2-0 kisha kwenda kupoteza kwa bao 1-0, lakini ikafuzu makundi ikipangwa Kundi A na kuburuza mkia.

Mwaka 2018 ilirudi kwa njia ileile ya kutemwa Ligi ya Mabingwa na kucheza mchujo safari hii ikiiondoa Welayta Dicha ya Ethiopia nyumbani ikishinda 2-0 na kupoteza ugenini 1-0, kisha kupangwa Kundi D na kumaliza tena mkiani.

ILIVYO TUNISIA

Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe anasema: “Mazoezi yetu tukiwa hapa yalienda sawa. Hakuna majeruhi yeyote yule na hata Sure Boy (Salum Abubakar) ambaye tulikuja naye akiwa anaumwa amejiunga na wenzake kwenye mazoezi na anaendelea vizuri.”

“Kuna viongozi walitangulia mjini hapa kuweka mazingira sawa na kila kitu kinaenda sawa hakuna tabu yoyote. Kikosi kipo kwenye hali nzuri na tunaenda kupambana na wachezaji wote morali ipo juu kwa ajili ya mchezo huu.”

REKODI YANGA UGENINI KIMATAIFA

Yanga haina rekodi nzuri sana inapokuwa ugenini upande wa kimataifa kwani mara ya mwisho kucheza mashindano ya Shirikisho 2018 ilitolewa hatua ya makundi ikishika nafasi ya mwisho kundi D ikiwa na pointi 4. Kwenye kundi hilo kulikuwa na timu moja kutoka Algeria ya USM Alger na Yanga ikiwa Uwanja wa Mkapa ilishinda 2-0, lakini mchezo wa marudiano nchini Algeria ilifungwa 4-0.

Upande wa mechi zingine za ugenini kwenye kundi hilo ilifungwa 4-0 na Gor Mahia na pia 1-0 na Rayon Sports. Mwaka 2016 ikiwa kundi A ilimaliza na pointi nne, huku Waarabu pekee wakiwa ni Mo Bejaia kutoka Algeria.

Yanga ilifungwa 1-0 na Mo Bejaia wakiwa ugenini lakini wakalipiza kisasi kwa Mkapa kwa bao 1-0 lililofungwa na Thaban Kamusoko. Yanga inaonekana kutokuwa bora sana ugenini kwani ilifungwa mabao 3-1 na Medeama ya Ghana na 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo. Mwaka 2011 Yanga iliishia hatua ya awali baada ya kutolewa na Dedebit kwa mabao 6-4. Yanga ikiwa kwa Mkapa ilitoka sare ya 4-4 na Dedebit lakini ugenini, Ethiopia ilifungwa mabao 2-0 na kutolewa.

Mwaka 2008 Yanga ilitolewa raundi ya kwanza baada ya kutoka sare 1-1 na Al Akhdar ya Libya na mchezo wa marudiano Libya ilifungwa bao 1-0.

Mwaka 2007 ilitolewa mapema na Al Merrikh ya Sudan baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu ya bila kufungana Uwanja wa Mkapa na mchezo wa marudiano Sudan walifungwa 2-0.

WADAU

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amemshauri Nabi kutokuwa muoga na kwamba anapaswa kuanza na washambuliaji wawili ili kutafuta zaidi mabao.

“Bado Yanga ina nafasi ya kusonga mbele. Uzuri ilitoka sare nyumbani, hivyo kule inahitaji bao kwanza kabla ya mipango mingine. Kwa kawaida ya timu nyingi za mataifa ya Kiarabu zikiwa nyumbani zinashambulia sana na kutaka bao la mapema. Hilo pia Yanga inatakiwa ilitumie kama fursa ya kushambulia ili ipate bao na kujilinda kwa umakini zaidi,” anasema Chambua.

“Ikimpendeza Nabi aweke washambuliaji wawili ambao watadhibiti safu ya ulinzi ya Africain kucheza kwa uhuru na pia haohao wanaweza kuipa mabao timu kutokana na kadri nafasi zitakavyotengenezwa.”

Kocha wa Kipanga FC ya Zanzibar, Hassan Abdulrahman aliyecheza na Africain mechi za mtoano Ligi ya Mabingwa na kutoka nao suluhu nyumbani, lakini ugenini timu yake ikafungwa mabao 7-0, ameipa ujanja Yanga kujipanga zaidi maeneo ambayo Waarabu hao ni hatari.

“Ni timu inayotumia mbinu tofauti, lakini tulipocheza nayo mechi zote mbili iliingia na mfumo wa 3-5-2, mfumo huo wanapenda kutumia kasi na nguvu. Wakiwa nyumbani wanakulazimisha sana ufanye makosa na pia kuna mambo mengi ndani na nje ya uwanja yanayoweza kuwatoa wachezaji mchezoni lakini wakijipanga vizuri wanaweza kushinda na kusonga mbele,” anasema Hassan.

Katika mchezo huo huenda Yanga ikaanza na kipa Djigui Diarra; mabeki Kibwana Shomari, Djuma Shaban, Dickson Job na Yanick Bangala; viungo Khalid Aucho, Feisal Salum, Stephane Aziz na Benard Morrison huku washambuliaji wakiwa Fiston Mayele na Herritier Makambo.

SOMA NA HII  UNAAMBIWA HUKO JANGWANI NI MWENDO WA SUPU TU ....... HERSI ATOA CHAPATI 5000