Home Habari za michezo BAADA YA KUSIKIA AZAM NA SINGIDA ZINAMFUKUZIA SAIDO…SIMBA NAO WAJIBU MAPIGO KIBABE…ISHU...

BAADA YA KUSIKIA AZAM NA SINGIDA ZINAMFUKUZIA SAIDO…SIMBA NAO WAJIBU MAPIGO KIBABE…ISHU YOTE IKO HIVI…

SIMBA ipo katika hatua za mwisho kunasa saini ya kiungo mshambuliaji wa Geita Gold na timu ya taifa ya Burundi, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa juzi Ijumaa na taarifa ni kwamba jamaa ameitwa fasta aje jijini Dar es Salaam kutoka Bunjumbura alipokuwepo.

Inaelezwa kuwa fundi huyo wa frikikii na mkali wa asisti, muda wowote kuanzia leo atatua jijini Dar es ili kuja kumalizana na kigogo mmoja wa Simba aanayesimamia dili lake na aliyekuwa nje ya nchi ambaye tayari amerejea nchini tangu juzi Alhamisi kutoka Qatar.

Awali mazungumzo baina ya Simba na staa huyo mwenye mabao manne na asisti sita yamefikia pazuri na inasemekana ameshatumiwa tiketi ili aje kutoka kwao Burundi kwa mapumziko na atapanda Ndege kuja Dar kumalizia dili hilo kwa kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Katika mazungumzo ya awali kati ya Saido na Simba walifikia makubaliano ya kumpa mkataba wa miaka miwili na kwa mshahara wa dola 3,500 (zaidi ya milioni saba za kitanzania), na pesa ya usajili isiyopungua Dola 25,000 ambazo ni zaidi ya milioni 50 za kibongo lakini hakusaini mkataba huo kutokana na matakwa mengine kusubiri kikao cha viongozi.

Chanzo cha ndani ya Simba kinasema kuwa sababu kuu ya Saido kushindwa kusaini mkataba awali ni matakwa ya nyumba, gari na kutokaa kambini jambo ambalo Simba imekubali kulikamilisha kwa mashariti na sasa imemuita Dar es Salaam aje wamalize kila kitu.

Simba imekubali kumpa nyumba ya kifahari nyota huyo katika moja ya maeneo kati ya Oysterbay, Mikochini au Masaki ambapo amependekeza yeye na kumpatia gari la kumpeleka mazoezini na kumrudisha lakini kuweka mashariti katika kipengele cha kutokaa kambini ambapo uongozi umepanga kumtaka kambini siku tatu hadi tano kabla ya mchezo kutokana na matakwa ya waalimu jambo ambalo litazungumzwa zaidi akishatua nchini.

Mwenyewe alipotafutwa kutoka Burundi, alisema kwa kifundi kwamba kila kitu kitakuwa hadharani baada ya kukamilika kwa dili alizonazo, bila kuainisha kama ni la Simba ama la.

“Kwa sasa nipo nyumbani Burundi nimepumzika, sipo na timu (Geita) kwa kuwa natumikia adhabu ya kadi nyekundu na kama kuna lolote zaidi mtajua muda ukifika,” alisema Saido anayemalizia mkataba wake wa miezi sita na Geita na kuongeza;

“Hizo ishu za usajili kwenye hili dirisha dogo, zitakuwa wazi kila kitu kikikamilika ila kwa sasa naomba nipewe muda kwanza.”

AZAM, SINGIDA NDANI
Wakati Simba ikikimbizana kuhakikisha Saido anakuwa usajili wao wa kwanza kwenye dirisha dogo hili, inaelezwa Azam na Singida Big Stars nazo zimeonyesha nia ya kutaka saini ya kiungo huyo na tayari zimetuma ofa kwa staa huyo wa zamani wa Ligi Kuu ya Ufaransa.

Inafahamika kuwa Singida ilianza kumuwinda Saido tangu mwanzo wa msimu huu kama ilivyokuwa kwa Simba, lakini ilimkosa kutokana na kutoa masharti magumu yaliyowafanya walima Alizeti hao kuachana naye na kumsaini Meddie Kagere katika dakika za mwisho lakini kiwango alichokionyesha akiwa na Geita kimewafanya wamtafute tena na inaelezwa amewapa bajeti ile ile ya mwanzo.

Kwa upande wa Azam nao wamewasiliana na Saido na kuwapa ofa yake lakini vigogo wa timu hiyo wamelazimika kurudi chimbo kuijuadili ofa ya kiungo huyo na huenda kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo wakamtumia ofa yao.

AAGWA GEITA
Tayari wachezaji na hata baadhi ya viongozi wa Geita, wamedaiwa kuanza kumuaga kiungo huyo na kocha wa kikosi hicho, Fred Felix ‘Minziro’, amekiri Saido ni kati ya wachezaji atakaowapoteza kikosini kwake baada ya dirisha dogo hili na tayari ameanza kutafuta nyota wengine wa kuziba nafasi ya Mrundi huyo na George Mpole aliyesajiliwa FC Lupopo ya DR Congo.

“Sina uhakika kama tutaendelea kubaki na wachezaji wetu wote hususani eneo la mbele kwani Mpole ameondoka na wengine akiwemo Saido wanaweza kuondoka,” alisema Minziro na kuongeza;

“Tutaangalia nini cha kufanya lakini lazima tuzibe nafasi zilizo na upungufu kwa kuongeza wachezaji katika maeneo muhimu ikiwemo pale mbele.”

SOMA NA HII  SPOTI XTRA LAMWAGA TIKETI KWA MKAPA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here