Home Habari za michezo MGUNDA: SIMBA SC HATAYUMBA KISA PHIRI HAYUPO…TUNAVIFAA VYA MAANA…

MGUNDA: SIMBA SC HATAYUMBA KISA PHIRI HAYUPO…TUNAVIFAA VYA MAANA…

Habari za Simba

Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda amethibitisha kuwa kinara wa mabao wa timu hiyo, Moses Phiri atakosekana katika mchezo wa leo dhidi ya KMC utakaopigwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Phiri mwenye mabao 10 na assiti mbili katika michezo 17 ya Ligi msimu huu aliumia katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1 katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ambapo katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hajaonekana.

Mgunda amesema hayo Desemba 25, 2022 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza, huku akiwatoa wasiwasi mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuwa kukosekana kwa nyota huyo hakutowaathiri kwenye mchezo wa leo kwani timu yao ina kikosi kipana chenye nyota wengi wanaoweza kuwapa furaha.

“Kweli Phiri alipata maumivu mchezo uliopita lakini anaendelea vizuri japokuwa katika mchezo wa kesho hatakuwepo, hakuna ugumu wowote juu ya kukosekana Phiri na sidhani kama timu itakosa morali kwa sababu hayupo,”

“Maandalizi ya mchezo wa kesho (leo) na wachezaji waliopo yako vizuri tuombe inshallah mambo yatakwenda vizuri, Simba SC tuna wachezaji wengi ambao wanaweza kutupatia matokeo,” amesema.

Akizungumzia mchezo huo, Mgunda amesema maandalizi yote yamekamilika na wamejiandaa vyema kuikabili KMC huku akitahadharisha kuwa utakuwa mtanange mgumu na wenye ushindani kwa sababu wanaiheshimu timu hiyo.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika tuko tayari kupambana na KMC utakuwa mchezo mgumu na mzuri wenye ushindani mkubwa kwani tunawaheshimu KMC, lakini tumejiandaa kushindana na kufanya vizuri,” ametamba Mgunda.

Kuhusu ujio wa Saido Ntibazonkiza na uwepo wake katika mchezo wa leo, Mgunda amesema “Saido ni mchezaji wetu na amesajiliwa kuja kuitumikia Simba SC, tumempokea vizuri na tunategemea ataongeza kitu akipata nafasi ya kuitumikia Simba SC atatimiza wajibu wake,”

Mchezo huo utakuwa wa 10 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi, ambapo katika michezo tisa ya nyuma Simba imeshinda nane na sare moja ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa haijapoteza michezo yake minne ya mwisho ugenini, ambapo iliichapa Polisi Tanzania 3-1, Coastal Union 3-0, Geita Gold 5-0 na sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

SOMA NA HII  TP MAZEMBE WAWASILI SALAMA TANZANIA