Home Habari za michezo UKICHEZA NA SIMBA HII….JIANDAE KWA LOLOTE AISEE…KAMA SI NYEKUNDU BASI NJANO INAKUHUSU…

UKICHEZA NA SIMBA HII….JIANDAE KWA LOLOTE AISEE…KAMA SI NYEKUNDU BASI NJANO INAKUHUSU…

Habari za Simba

Timu pinzani zinazocheza na Simba kwa sasa zinapaswa zijiandae kabisa kucheza zikiwa pungufu, kwani rekodi zinaonyesha robo ya mechi za timu hiyo zimesabababishia wapinzani kadi nyekundu.

Ndio, Simba ni timu iliyosababisha kadi nyingi nyekundu kwa wapinzani wake katika mechi inayozihusisha timu hiyo, kwani kati ya kadi 20 zilizoonyeshwa hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara, timu hiyo imehusika na sita, zikiwamo tano zilishowaponza wapinzani na moja inayohusu wenyewe.

Rekodi zinaonyesha hadi sasa katika ligi iliyopo raundi ya 20, jumla ya kadi nyekundu 20 zimeonyesha, huku wachezaji wa Polisi Tanzania wakiwa vinara wa kupata kadi nyingi kwani hadi sasa timu hiyo imevuna kadi tano, huku Simba ikiwa kinara dhidi ya wapinzani wake.

Katika mechi iliyofanyika Septemba 14, 2022 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Jamal Masenga wa Prisons alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90+1 na mwamuzi Ahmed Arajiga baada ya kumkwatua Moses Phiri katika mchezo ambao Simba ilishinda bao 1-0.

Mtibwa Sugar nayo haikupona dhidi ya Simba baada ya wachezaji wake wawili, Pascal Kitenge na Cassian Ponera kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliofanyika Oktoba 30 mwaka jana kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa na kumalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kushinda mabao 5-0.

Wachezaji hao walionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Tatu Malogo kwa makosa tofauti, baada ya Kitenge kumuangusha Pape Sakho dakika ya 41 na Ponera dakika ya 67 baada ya kumvuta jezi Augustine Okra wakati akielekea eneo la hatari.

Simba nayo msimu huu hadi sasa imepata kadi nyekundu moja iliyokwenda kwa kiungo Sadio Kanoute katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa na wageni kushinda mabao 3-0

Timu hiyo pia iliendelea kuwapa umeme wapinzani wao kwani Samson Mbangula wa Prisons naye alilimwa kadi nyekundu na mwamuzi Abdul Wajih baada ya kumfanyia madhambi Henock Inonga dakika ya 20 katika mchezo uliofanyika Desemba 30 Kwa Mkapa na Simba kushinda mabao 7-1.

Pia katika mchezo uliofanyika Januari 18 mwaka huu, Samson Madeleke wa Mbeya City alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Ester Adalbert baada ya kumfanyika madhambi Sakho.

POLISI SASA

Hadi sasa Polisi ndio inaongoza kwa wachezaji wake kupata kadi nyekundu ambao ni Ibrahim Hilika dhidi ya Ruvu Shooting (Januari 2, 2023), Rajab Athuman v Namungo(Januari 14, 2023), Ambrose Awio v Yanga (Desemba 17, 2022), Mohamed Mmanga v Ruvu Shooting (Septemba 19, 2022) na dhidi ya Yanga (Agosti 16, 2022)

Wachezaji wengine waliopata kadi nyekundu hadi sasa msimu huu ni; Collins Opare (Dodoma Jiji) , Abdul Omary, Emmanuel Asante (Namungo), Rodgers Kola (Azam FC), David Kameta, Charles Ilanfya (Mtibwa Sugar), Adeyum Saleh (Geita Gold), Juma Nyosso (Ihefu), Benedict Haule (Singida BS) na Saidi Ntibazonkiza (Geita Gold/ Simba)

Wasikie makocha

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema hakuna mchezaji ambaye huwa anatumwa kutafuta kadi nyekundu uwanjani, lakini kunamatukio ambayo huwafanya kukumbana na adhabu hiyo, “Binafsi huwa nawaambia wachezaji wangu hakuna kumwachia mtu mwanya wa kutuletea madhara, huwa mkali kwenye hilo,” alisema Maxime na kuongeza;

“Kuonyeshwa kadi nyekundu ni sehemu ya mchezo, huwa sipendi kadi za kizembe lakini ile ya kimchezo huwa inakubalika, imetokea tu kwa Simba lakini sio kwamba wao hukamiwa sana kuliko timu nyingine.”

Upande wa kocha wa Dodoma Jiji, Melis Medo alisema; “Ni ngumu muda mwingine kudhibiti matukio ya kadi nyekundu, ila huwa tunawaandaa wachezaji kuwa na nidhamu ya mchezo, nadhani miili ikishapata moto huwa kuna matukio mengine wanashindwa kujizuia, hakuna mwalimu anayefurahia timu yake kucheza pungufu.”

Kocha mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru ambaye mchezaji wake Samson Madeleke alipata kadi nyekundu kwenye mechi iliyopita dhidi ya Simba alisema kuna baadhi ya maamuzi yanayotolewa kimakosa. “Binafsi kuna maamuzi siyafurahii kutokana na kutolewa kimakosa lakini ndio mpira siwezi kusema mengi juu ya hilo,” alisema Mubiru.

SOMA NA HII  BOCCO ATAMBA NYUMBANI MATOKEO MAZURI UHAKIKA