BAADA ya kurejea nchini akitokea kwao Brazil, Kocha Mkuu wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amekabidhiwa faili la wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Horoya na mabosi wake tayari kwa kuanza kusaka ushindi.
Robertinho ambaye amerejea nchini juzi akitokea kwao Brazil alipokwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia kabla ya leo kukaa kwenye benchi katika mchezo Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Big Stars katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya timu zinaeleza kuwa kabla ya kuondoka kwa kocha huyo aliacha maagizo kwa mabosi wa timu hiyo kumtafutia mambo muhimu ya wapinzani wao katika hatua ya makundi ili kuweza kujiweka sawa kabla ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya Horoya ya Guinea katika mchezo wa kwanza wa kundi C utakaopigwa Februari 11, mwaka huu nchini Guinea.
Mtoa taarifa ameenda mbali kwa kusema kuwa tayari kocha huyo ameshapewa kila kitu juu ya wapinzani wao wao kabla ya kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo huo ambao anataka kuona anaweka rekodi ya kushinda ugenini.
“Ni kweli kocha amepewa faili la Horoya kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kwa sababu yalikuwa ni maagizo yake ili ajue katika maandalizi yake wanafanya nini ili kuweza kupata ushindi ugenini.
“Lakini hili ni jambo ambalo anataka linakuwa endelevu kwa kuwa kila mchezo timu zinakuwa na mbinu tofauti hivyo bado anaendelea kupewa taarifa nyingi hasa wapinzani wanapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani na baada ya mchezo na Singida kila kitu atakielekeza kwenye michuano hiyo,” alisema mtoa taarifa.
Alipotafutwa kocha huyo ambaye alisema kuwa kwa sasa mipango yake ni kuhakikisha wanapata matokeo katika mchezo wa leo Ijumaa dhidi ya Singida kabla ya kuelekea nguvu kwenye michuano ya kimataifa.