Home Habari za michezo BAADA YA KUONA VIPERS WAMEBONDWA JANA…MBRAZILI SIMBA AIBUKA NA HILI JIPYA KWA...

BAADA YA KUONA VIPERS WAMEBONDWA JANA…MBRAZILI SIMBA AIBUKA NA HILI JIPYA KWA HOROYA…

Habari za Simba leo

Simba wanaanza leo.  Saa 1 kamili usiku, usibanduke kwenye kiti chako wala usiguse rimonti. Kocha Oliveira Robertinho amewaambia mashabiki wa Simba na wadau wa michezo watembee kifua mbele. Wanawamudu Horoya AC hata kama wako kwao Guinea.

Kocha huyo aliyetua Msimbazi hivi karibuni akitokea Vipers ya Uganda iliyopo pia kundi hilo, amesema kwamba, licha ya mechi hiyo kuonekana ngumu, lakini kwa kazi kubwa aliyofanya na vijana wake anadhani wataimaliza mapema kwenye Uwanja wa General Lansana Conte, jijini Conakry.

Simba itavaana na wenyeji hao ikiwa ni mara ya kwanza kukutana kwenye michuano ya CAF, kocha huyo akikabiliwa na mtihani wa kuibeba timu hiyo baada ya kazi kubwa iliyofanywa na msaidizi wake, Juma Mgunda aliyeingiza makundi.

Robertinho alisema ujanja aliutumia wa kuisoma timu hiyo mapema mara baada ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara akimtumia mtaalamu wao kutoka Zimbabwe, Calvin Mavunga, imemsaidia kujua pa kuanzia na kwa mazoezi aliyoyafanya anaona kabisa wanatoboa ugenini.

“Najua ni timu yenye kushambulia sana inapokuwa nyumbani ili kutaka kutoka na ushindi, pia wapo imara eneo la kiungo, lakini tayari nimeshawaandaa wachezaji wangu kuhakikisha wanakabiliana na kila kitu ili kuanza vyema mechi hii ya kwanza na ya ugenini,” alisema Mbrazili huyo na kuongeza;

“Bahati nzuri hata sisi tuna timu nzuri katika maeneo yote hivyo tupo tayari kupambana na niwahakikishie mashabiki kwamba Simba itawapa raha, kwa vile malengo yetu ni kufika mbali zaidi na hatua tuliopo sasa.”

Kwa upande wa mshambuliaji na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco wako makini na hawana presha yeyote kutokana na mechi wanayoenda kukutana nayo huku akikiri kuwa mchezo huo utakuwa ni mgumu kwa pande zote.

“Tunatarajia kukutana na mchezo mgumu lakini mwisho wa siku maandalizi yetu ndio yanaweza kwenda kutupa matokeo chanya, tunawaomba watanzania wapenda mpira na mashabiki zetu wa simba waweze kutuombea na kutupa sapoti.”

Simba itavaana na Horoya bila nyota watano akiwamo Saido Ntibazonkiza, Jonas Mkude, Jimmyson Mwanuke, Augustine Okrah na Peter Banda wenye matatizo tofauti, lakini bado ina majembe ya maana miongoni mwa wachezaji 24 waliosafiri hadi Conakry.

Baadhi ya nyota wanaotegemewa kuibeba timu leo na ambao wanaweza kuanza kikosi cha kwanza ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Ismael Sawadogo, Jean Baleke, Clatous Chama na Pape Ousmane Sakho. Pia kuna Moses Phiri, John Bocco, Kibu Denis, Habib Kyombo, Israel Mwenda, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Kennedy Juma.

Katika kundi C la Simba kinara ni Raja Casablanca ya Morocco ambayo ina pointi tatu baada ya jana kushinda mabao 5-0 dhidi ya Vipers ya Uganda.

SOMA NA HII  MFAHAMU SHABIKI HUYU KIPOFU WA SOKA...HAJAWAHI KUKOSA UWANJANI