Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA WAARABU LEO…MUDATHIRI KUPEWA ‘HIRIZI ZA YANGA’…

KUELEKEA MECHI NA WAARABU LEO…MUDATHIRI KUPEWA ‘HIRIZI ZA YANGA’…

Habari za Yanga

Yanga juzi imeanza mazoezi yake ya kwanza ndani ya ardhi ya Tunisia baada ya kufika tayari kwa kuwavaa wenyeji wao, US Monastir, lakini kuna kitu Kocha Nasreddine Nabi anataka kifanywe na kiungo wake mmoja na kama wakifanikiwa, basi mashabiki wao watatamba sana.

Iko hivi. Yanga baada ya kufika Tunisia jioni yake walitoka na kwenda kufanya mazoezi flani ya ‘rikavari’ maalum kwa ajili ya kurudisha nguvu ya mwili kuwa katika utulivu mkubwa.

Mazoezi hayo yalifanyika katika jumba maalum la kisasa lenye joto kali ndani tofauti na hali ya baridi iliyopo nje ya jengo hilo ambapo wachezaji walikaa kwenye chumba na kufanya mazoezi kwenye maji kama sauna flani hivi.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema tofauti na mechi iliyopita nchini humo dhidi ya Club Africain waliyoing’oa, hali ilikuwa ya joto tofauti na sasa kuna baridi kali lakini Nabi alitumia ujanja kuidhibiti mapema kwa mastaa wake ili kuiweka miili sawa na kuizoea.

Mazoezi hayo yalifanyika kwa umakini mkubwa chini ya Kocha Msaidizi, Cedric Kaze akisaidiana na Helmy Gueldich mtaalam wa mazoezi ya viungo huku wakimsubiri kocha wao mkuu, Nasreddine Nabi ambaye alikuwa anatokea mji mwingine alikokwenda kuwasoma wapinzani wao Monastir waliokuwa wanacheza ugenini dhidi ya vibonde Rejiche wakishinda kwa mabao 2-0, ukiwa ni mchezo wa ligi.

Juzi asubuhi timu hiyo ilirudi uwanjani kwa mara ya kwanza ikijifua kwa saa 2:20 katika moja ya uwanja bora uliopo jijini Tunis.

Hata hivyo, katika mazoezi hayo Nabi akiwa kazini alionekana kufanya kikao maalum ndani ya uwanja na kiungo wake mkabaji Mudathir Yahya huku baadaye akimpa kazi maalum ya kucheza kwa mkakati mkubwa.

Nabi anataka Mudathir kutembea mguu kwa mguu na kiungo mmoja fundi wa Monastir ambaye ndiye injini ya mashambulizi makali ya timu yao kutokea katikati ya uwanja.

Kocha huyo anaamini Mudathir ndiye mtu sahihi ambaye anaweza kuhakikisha wakimkamata huyo basi mambo mengine yatakuwa sawa kusaka ushindi katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili Februari 12.

Aziz KI, Job wajazwa minoti Wakati hesabu za Yanga uwanjani zikianza hivyo mabosi wa timu hiyo tayari walishamaliza kazi hata kabla ya kikosi chao kupanda pipa, wakamalizana nao kwa malipo yao yote ya posho zao zote za mechi zilizopita.

Mzuka huo ulionekana kuwafurahisha makocha wa timu hiyo kwa hamasa kubwa ya morali iliyoonekana katika mazoezi ya jana kila mchezaji akionekana kuitaka mechi hiyo kwa kupambana zaidi mazoezini.

Yanga iliyopo Kundi D ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho itashuka uwanjani kesho jijini Tunis kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kuvaana na TP Mazembe ya Dr Congo na mechi itakayofuata itakuwa ugenini dhidi ya Real Bamako ya Mali Februari 26.

SOMA NA HII  MABEKI YANGA WAKINGIWA KIFUA,SABABU YA KUFUNGWA YATAJWA