Home Habari za michezo BAADA YA KUPIGWA CHA ‘UCHUNGU JUZI’…MPANGO WA SIMBA KWA WAARABU UKO HIVI…

BAADA YA KUPIGWA CHA ‘UCHUNGU JUZI’…MPANGO WA SIMBA KWA WAARABU UKO HIVI…

Kikosi cha Simba

SIMBA juzi Jumamosi ilianza vibaya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kulala bao 1-0 ugenini mbele ya Horoya ya Guinea, lakini benchi la ufundi likawaambia mashabiki wa timu hiyo ‘Tukutane kwa Mkapa’ watakapovaana na Raja Casablanca.

Uwanja wa Mkapa umekuwa kama machinjioni kwa timu pinzani zinazocheza na Simba kwani imekuwa ikitoka na ushindi, licha ya mwaka jana kubutuliwa na Jwaneg Gallaxy ya Botswana baada ya kukaa miaka minane bila kupoteza tangu ilipofungwa na Recreativo do Libolo ya Angola mwaka 2013.

Simba ilikumbana na kipigo hicho kwenye mechi ya Kundi C iliyopigwa Uwanja wa General Lassana Conte, mjini Conakry, huku kipa Aishi Manula akiokoa penalti kipindi cha pili na kunusuru aibu zaidi.

Manula, alipangua penalti hiyo dakika ya 72 iliyopigwa na mfungaji wa bao pekee la Horoya Pape Ndiaye baada ya beki Joash Onyango kuunawa mpira langoni mwa lango la Simba.

Mbali na kupangua penalti hiyo na kuwa kona isiyozaa matunda, Manula alifanya kazi ya ziada kwa dakika 90 kuokoa hatari zilizoelekezwa na wenyeji ambao walicheza soka la kushambulia na kukaba kwa pamoja.

Matokeo hayo ya juzi yameifanya Simba kushika nafasi ya tatu ikitanguliwa na vinara Raja yenye pointi tatu na mabao matano, huku Horoya ikiwa ya pili kwa alama kama hizo ila ikiwa na bao moja na Vipers ya Uganda ikiburuza mkia kundini.

Katika mchezo huo, wachezaji wanne wa Simba, Mohammed Hussein, Sadio Kanoute, Joasha Onyango na nahodha Joha Bocco aliyeingia kipindi cha pili walionyesha kazi za njano.

Kadi aliyopewa Kanoute imemfanya aukose mchezo wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa wakati Simba ikiikaribisha Raja.

Simba iliuanza mchezo huo kwa kucheza na tahadhari, Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akiwaanzisha viungo wakabaji watatu kati, Kanoute, Ismael Sawadogo na Mzamiru Yassin, ikifanya mashambuli machache tofauti na soka lililozoeleka.

Eneo la mbele Mbrazili huyo alimunzisha Jean Baleke, Clatous Chama na Pape Ousmane Sakho ambaye hakuwa na makeke kiasi cha kutolewa kipindi cha pili kumpisha Bocco.

Iliwachukua dakika 18 tu kwa Horoya kupata bao baada ya Ndiaye kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona mbele ya Henock Inonga.

Simba ilicharuka na kutaka kusawazisha bao hilo, lakini dakika 45 za kwanza ziliisha ikiwa nyuma kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Robertinho alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Sakho na baadaye Baleke na kuwaingiza Bocco na Denis Kibu, kiasi cha kuongeza kasi ya mashambulizi na kukosa mabao mawili ya wazi mara baada ya Horoya kupoteza penalti dakika ya 72.

Bocco alipoteza nafasi mbili za wazi ikiwamo aliyopenyezwa pasi tamu na Chama lakini alizidiwa maarifa na beki wa Horoya, Samassekou aliyeuondosha mpira huo kwenye hatari.

Dakika za lala salama tena Bocco na Kibu walipoteza nafasi na kufanya mchezo uishe kwa Mnyama kuanza vibaya kwa kulala bao 1-0.

Simba ilitarajiwa kuanza safari kurudi nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya Wamorocco, huku Kocha Robertinho alisema watajipanga vyema baada ya kuteleza jana kwa kutotumia nafasi walizopata.

Vikosi vilivyoanza;

HOROYA: Moussa Camara, Salif Coulibaly, B. Samassekou, Issaka Samake, Khadim Diaw, Mory Kante, Fode Camara, Mohamed Wonkoye, Alseny Soumah, Pape Ndiaye, Daouda Camara.

SIMBA:Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hennock Inonga, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Ismael Sawadogo, Mzamiru Yassin, Pape Sakho, Jean Baleke na Clatous Chama.

SOMA NA HII  ALLY KAMWE:- SIMBA vs AZAM SITAKI MTU AFUNGWE...ILA IKIBIDI BASI AHAMED ALLY ATALIA...