ACHANA na kauli ya kuutaka ushindi wa mchezo wa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo hata hivyo walifungwa kwa goli 3-0, lakini kuna kitu kikubwa tajiri wa Simba, Mohamed ‘MO’ Dewji amewapasha mastaa wa timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu huu baada ya kufanya kikao cha dharura.
Katika kikao chake kilichofanyika juzi, MO Dewji aliwataka wachezaji kushinda mechi ya juzi dhidi ya Raja Cassablanca, lakini ujumbe wake ni kwamba ushindi huo uanzishe safari yao ya kuelekea robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kufikiria hatua nyingine za juu zaidi.
MO, aliyepewa cheo cha rais wa Heshima wa Simba, aliwaambia wachezaji kwa kikosi kilichopo baada ya kumaliza usajili wa dirisha dogo Januari hatua ya kufika robo fainali ni lazima waitimize.
Tajiri huyo aliongeza kuwa katika kushiriki kwao mashindano mapya ya CAF Super Cup haitakuwa na maana kama watashindwa kufika hatua ya robo fainali kwa mara nyingine.
“Mimi na uongozi mzima wa Simba na mashabiki wetu tunawaamini na hata ninyi mnaona hakuna kinachoshindikana, sitaki mfikirie fedha nataka mfikirie zaidi mafanikio ya Simba kufika robo fainali,” alisema MO aliyeongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na wajumbe wengine wa bodi hiyo kwenye kikao hicho na wachezaji kambini.
“Tunahitaji kufika hapo tena kwa mara nyingine na baada ya hapo tutaangalia hesabu zinaturuhusu vipi, Simba ni kubwa tukathibitishe ukubwa wetu kuanzia mechi hii.”
Simba ipo nafasi ya nne katika Kundi C la michuano hiyo sambamba na Raja, Horoya na Vipers na timu mbili za juu za kundi hilo zitafuzu hatua ya robo fainali.