Home Habari za michezo KISA UDHAIFU WA REAL BAMAKO…MAYELE AIONA ROBO FAINAL CAF…

KISA UDHAIFU WA REAL BAMAKO…MAYELE AIONA ROBO FAINAL CAF…

Habari za Yanga

Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele anaamini AS Real Bamako inaweza kuwa msaada mkubwa kwa Yanga kufikia lengo la kucheza Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Yanga leo Jumapili (Februari 26) itacheza mchezo wake watatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho ikiwa ugenini mjini Bamako-Mali dhidi ya AS Real Bamako, katika Uwanja wa Machi 26 saa moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Mayele ametoa kauli hiyo kwa kuamini kama wakishinda mchezo huo, Yanga itakuwa na nafasi nyingine ya kipekee ya kupambana nyumbani Dar es salaam kwenye michezo miwili mfululizo dhidi ya AS Real Bamako na US Monastir, ambayo anaamini wanaweza kushinda na kuambulia alama nyingine sita.

Mshambuliaji huyo amesema jambo la msingi kwao ni kupambana kwenye mchezo wa leo Jumapili, na kusaka alama tatu, ili iwe rahisi kwao kufikia lengo la kufuzu Robo Fainali mapema.

“Tunafahamu ni kwa jinsi gani kama tukipata matokeo mazuri ya ushindi tukiwa ugenini tutakuwa na nafasi ya kufuzu kwenda Robo Fainali, nasema hivyo kwa kuwa kama tukishinda hapa Mali tutakuwa na michezo miwili mfululizo nyumbani Tanzania.”

“Hivyo itakuwa faida kubwa sana kwetu kuzipata na tutakuwa tumejipa nafasi nzuri ya moja kwa moja kufuzu. Sisi kama wachezaji tayari tumeshaongea na tumekubaliana kuwa tupambane kama ambavyo tulivyofanya dhidi ya TP Mazembe.”

“Tunatambua kuwa huu ni mchezo mgumu sana kwetu kwa kuwa ukiwaangalia Real Bamako wanatafuta ushindi, kwa sababu walipoteza mchezo wao wa kwanza wakiwa ugenini, kisha walipata sare wakiwa hapa kwao, na sasa wapo kwao tena, hawatakuwa tayari kurudia makosa, ndio maana ninasema mchezo huu utakua mgumu sana,” amesema Mayele

Baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe jijini Dar es Salaam, Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia yenye alama nne.

TP Mazembe ipo nafasi ya tatu kwa kuwa na alama tatu, huku AS Real Bamako iliyoambulia matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya US Monastir ikiburuza mkia wa Kundi hilo kwa kuwa na alama moja.

SOMA NA HII  BANGALA AFUNGUA KILA KITU, KUHUSU KUTUA AZAM, AWATAJA MAXI, SKUDU, TUHUMA ZAKE NA SIMBA