Home Habari za michezo KISA TP MAZEMBE…NABI APANGA KUPIGA PANGA LA MAANA KWA MASTAA YANGA…ISHU IKO...

KISA TP MAZEMBE…NABI APANGA KUPIGA PANGA LA MAANA KWA MASTAA YANGA…ISHU IKO HIVI..

Habari za Yanga

Yanga kuelekea mchezo wa pili wa Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi amepanga kukifumua kikosi chake.

Yanga itavaana dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa Kundi D, Yanga itaingia uwanjani ikiwa na hasira ya kutoka kufungwa bao 1-0 dhidi ya US Monastir ugenini nchini Tunisia.

Mmoja wa mabosi wa Benchi la Ufundi la Yanga, ameliambia Spoti Xtra kuwa mabadiliko machache yatakuwepo katika mchezo huo kutoka cha kile ambacho kilicheza dhidi ya US Monastir.

Bosi huyo alisema kuwa katika mchezo dhidi ya TP Mazembe, ataingia kuucheza kiufundi zaidi kwa kuwatumia wachezaji wenye uwezo wa kushambulia na sio kujilinda sana.

Aliongeza kuwa, upo uwezekano wa kumuanzisha beki wa kushoto Joyce Lomalisa akichukua nafasi ya Kibwana Shomari, Farid Mussa akiingia kikosini kuchukua nafasi ya Tuisila Kisinda ambaye alicheza katika kiwango kidogo dhidi ya US Monastir.

“Kuelekea mchezo wetu wa pili wa Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ipo mikakati mikubwa inayopangwa kwa kuanzia uongozi, wachezaji na benchi la ufundi.

“Katika kutambua umuhimu wa mchezo huo, ni lazima benchi la ufundi wafanye mabadiliko ya kikosi kwa kuwaondoa wachache ili wengine waingie kwa ajili ya faida ya timu na kikubwa kupata ushindi.

“Lomalisa ana nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo dhidi ya Mazembe, kwani ni mzuri katika kutengeneza mashambulizi katika goli la wapinzani na uzuri zaidi hatuhitaji kujilinda zaidi tukiwa nyumbani.

“Lakini tukiwa ugenini ni lazima tucheze kwa tahadhari kubwa ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushitukiza, pia Farid ana nafasi ya kuanza akichukua nafasi ya Kisinda aliyecheza chini ya kiwango,” alisema bosi huyo.

Nabi alizungumzia mikakati ya mchezo dhidi ya Mazembe kwa kusema kuwa: “Nimeona upungufu wa kikosi changu tulipocheza na US Monastir, kikubwa nimepanga kukifanyia maboresho katika baadhi ya maeneo.

“Mabadiliko ya kikosi ni lazima yawepo, hiyo ni baada ya kumuona mpinzani wangu, hivyo yatakuwepo maingizo mapya kuelekea mchezo dhidi ya Mazembe.”

Kikosi cha Yanga kilichoanza dhidi ya US Monastir ni Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Salum Aboubakari ‘Sure Boy’, Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki, Tuisila Kisinda.

SOMA NA HII  USAJILI WA SIMBA, YANGA SIO POA MNYAMA ATANGAZA KUMSAJILI KIUNGO HUYU WA AL HILAL YA SUDAN